Wajanja sekta ya ardhi wawapiga  hadi mawaziri na wabunge

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2024 / 2025, jijini Dodoma. Picha na maktaba

Muktasari:

“Mheshimiwa Spika naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu inatosha.”

Dodoma. Unaweza kusema kuti la mazoea limemuangusha mgema, msemo unaoendana na kile kinachowakuta wabunge, manaibu waziri na mawaziri kupigwa viwanja na wajanja.

Pengine walijua wanaopigwa ni wanyonge peke yao na kuchelea kuwabaini na kuwakomesha wachache waliokuwa na tabia hiyo, wamekubuhu sasa wanawatapeli hadi watunga sheria wa nchi.

Hali hiyo imemsukuma Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa kulieleza Bunge kuwa: ‘Imetosha.’

“Mheshimiwa Spika naomba kulitaarifu Bunge lako Tukufu inatosha.”

Ni kauli ya Waziri Silaa wakati akifanya majumuisho ya hoja za wabunge kwenye bajeti ya wizara hiyo ambayo imeongezeka kutoka Sh163.17 bilioni hadi Sh171.37 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025. Bunge limepitisha bajeti hiyo.

 Silaa amesema kliniki ya migogoro ya ardhi anayoifanya sasa ataongeza kasi, itakwenda kila mahali na itaitwa ‘Samia ardhi kliniki.’

Amesema licha ya upungufu wa watumishi katika Wizara ya Ardhi,  wanaohusika mahakamani, bungeni na serikalini ni binadamu na wana upugufu wao.

“Dhuluma, matapeli kwenye ardhi wamekithiri lazima tuende kuwasikiliza wananchi kutatua matatizo yao,” amesema.

Alizungumzia mfano uliotolewa na Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constatine Kanyasu kuhusu watumishi wa ardhi kutengeneza ramani feki na kumsaidia tapeli wa ardhi kushinda kesi mahakamani.

“Kanyasu amesema yuko mtu kaghushi ramani kaipeleka mahakamani. Tumeona watu wenye nguvu wenye ufundi wa kisheria kwenda mahakamani kuzuia mtu mwenye haki asipate yake, tuko tayari kutofautiana na baadhi ya maamuzi ya kutoa haki,” amesema.

Ametoa mfano wa kesi ya dhulma ya nyumba iliyochukua miaka 26 kwa sababu ya utapeli.

“Bunge, mahakama, Serikali kote kuna binadamu. Spika mahakama yetu inafanya kazi nzuri sana, lakini kesi ile imechukua miaka 26, hata wasiosoma sheria wangeona haki yao wangeipata miaka 26 iliyopita.

“Mawakili nao ni binadamu, wako mawakili wazuri, lakini wako mawakili wanaingiza wateja kwenye matatizo na kukosa haki zao,” amesema.

Waziri Silaa amesema Rais Samia Suluhu Hassan, amewapa maelekezo twende tukatende haki kwa Watanzania kwenye ardhi.

“Simamieni haki za watu kwenye ardhi ndiyo msingi wa kila kitu, ardhi ndio utajiri wa wananchi na kila kitu ni ardhi,’ amemnukuu Rais Samia.

Pia, ametangaza bungeni kuvunja masijala ya ardhi ya halmashauri ya Jiji la Dodoma na kuanzia leo (jana) na kuwataka watumishi wote kuripoti kwa kamishna msaidizi wa ardhi Mkoa wa Dodoma.

“Kauli  ya mheshimiwa mbunge amewasemea wabunge wengine hapa ndani, mheshimiwa Spika mwenyewe ni mwathirika wa vitendo vya baadhi ya watumishi wa Dodoma kwenye sekta ya ardhi, yuko mheshimiwa waziri mmoja hapa naye ni mwathirika, wako manaibu waziri sita nao ni waathirka, wako wabunge zaidi ya 30 na wenyewe wamepata madhara,” amesema.

Hoja za wabunge

Awali, wakichangia bajeti hiyo, Kanyasu amesema kuna mtu alitumia ramani feki kushinda kesi mahakamani kwa kumdhulumu mtu ardhi yake.

“Mfano, watu wa Takukuru  (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), walifanya uchunguzi, mtu mmoja kuanzia baraza la ardhi mpaka mahakama iliamua anyang’anywe ardhi, lakini kumbe watu wako walipeleka ramani feki kutoa ushahidi ikasababisha yule mwananchi ashindwe,” amesema.

Mbunge wa Singida Kaskazini, Abeid Ighondo, amesema tatizo la migogoro ya ardhi linatokana na watendaji walio chini ya wizara yake hasa katika ngazi ya wilaya ndio kunakotakiwa kumulika hasa.

“Nazungumzia ule uaminifu wa watumishi wetu hasa katika Jiji la Dodoma, ninatoa ushauri sana hapa kwa watendaji wa ardhi, waziri aangalie idara ya ardhi katika Jiji la Dodoma kuna matatizo makubwa, ndio chanzo cha migogoro ambayo wananchi wanakosa haki zao, wananyang’anywa ardhi zao kwa usimamizi wa watendaji wa ardhi.

“Na wao wanajigeuza kuwa wanasheria, wanajigeuza kuwa ni madalali, sasa hili jambo linakera wananchi wanakwenda na ‘genuine cases’ (mashauri ya kweli) lakini haziendi mpaka mwisho ni danadana tupu.

“Nimuombe sana waziri amulike sana eneo hili linakuchafua na linachafua kabisa taswira hata ya mheshimiwa Rais ambaye amesimama kuhakikisha wananchi wanatendewa haki na wananchi wengi wanakuwa ni wanyonge,” amesema.

Naye mbunge wa Momba (CCM) Condester Sichalwe amesema matatizo ya migogoro ya ardhi yamo ndani ya Wizara ya Ardhi na  kama  Waziri akitaka kuendelea na kliniki ya ardhi, basi  aruke na ndege wanaofanana, akimaanisha kuwaondoa watumishi wanaojihusisha na migogoro ya ardhi.

“Lakini, migogoro hii ya ardhi inapoibuka tulitegemea watumishi wa ardhi wawe kama mahakama kuzuia hiyo migogoro au ikiwezekana kusitisha isiwepo kabisa.

“Lakini ndani ya wizara yako wako baadhi ya watumishi ambao wao siyo waaminifu kwa uchu wao wa madaraka, kutaka kujipatia pesa haraka haraka wameendelea kuwa chanzo cha kuchochea migogoro hapa nchini kwa wenzao,” amesema.

Naye mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Profesa Patrick Ndakidemi,  amesema ndani ya wizara kuna watu wanakwamisha juhudi zake na kueleza alivyokutana na mwanamake nje ya Bunge aliyemtaja kwa jina Elizabeth Donald Mboji.

Mwanamke huyo ambaye ni  ni mlemavu alikuwa akimtafuta Silaa akilalamika watumishi wa ardhi kukaidi maagizo ya Waziri wa Ardhi ya kumpa ardhi yake.

“Na wewe uliishasema apewe eneo lake, sasa kama kuna mtu mkubwa kuliko wewe tunataka tujue,” amesema.

Mbunge wa Nungwi, Simai Hassan Sadik,  amesema haki ya kumiliki ardhi nchini inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ongezeko la idadi ya watu, upanukaji wa miji kiholela  na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Amesema suluhisho la changamoto hizo ni wizara hiyo kuwa na sera na sheria bora, ambazo utungwaji wake unatakiwa kuwashirikisha wananchi kwa kutoa maoni yao.

“Jambo hili la utungaji wa sera na sheria ni jambo zito na linahitaji mijadala ya Taifa, kama tulivyokuwa na Tume ya Haki Jinai,  basi umefikia wakati sasa hivi tuwe na Tume ya Haki Ardhi kutokana na unyeti wa jambo lenyewe,”amesema Simai.