Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wajapan kufanya upasuaji mtoto wa jicho wa aina yake Muhimbili

Dar es Salaam. Timu ya madaktari bingwa kutoka Japan imeweka kambi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) mahsusi kwa ajili ya kufanya upasuaji wa kitaalamu wa kuondoa mtoto wa jicho bila kupasua jicho.

Wagonjwa 30 wanatarajiwa kufanyiwa matibabu hayo ambayo yatafanyika kwa siku tatu.

Upasuaji huo utahusisha sindano maalumu ambayo itanyonya ukungu unaosababisha mtoto wa jicho (cataract) na kumuacha mgonjwa bila kidonda.

Daktari bingwa wa upasuaji wa macho wa MNH, Neema Daniel alisema jana kwamba madaktari hao watatumia utalaamu wa hali ya juu na kwamba mara baada ya tiba hiyo, mgonjwa ataanza kuona siku hiyohiyo.

“Huu ni utaalamu wa hali ya juu kabisa katika upasuaji macho, mgonjwa atafanyiwa na hatapata kidonda na ataona siku hiyohiyo.

“Badala ya kupasua kama sisi tunavyofanya, wanatumia mbinu hii mpya ni ya kunyonya. Wananyonya kioo cha jicho kilichopata ukungu (mtoto wa jicho), kisha wanaweka kingine kwa kuchoma na sindano badala ya kupasua,” alisema Dk Neema.

Alisema wagonjwa 15 watafanyiwa upasuaji siku ya kwanza na wengine 15 siku inayofuata.

Dk Neema ambaye pia ni mkuu wa kitengo cha macho katika hospitali hiyo alifafanua kuwa upasuaji huo unahusisha mashine za kitaalamu (pheco machine) ambazo hazipo nchini. “Tunatamani watuachie, lakini hata wakituachia inabidi wanaozitumia wapatiwe ujuzi kwanza kwa sababu ni za kitaalamu sana,” alisema.

Alisema ugonjwa wa mtoto wa jicho ndiyo unaoongoza kwa magonjwa ya macho.

“Cha kushukuru ni kwamba ndiyo ugonjwa wa macho unaopona kwa asilimia 100, ukilinganisha na magonjwa mengine ya macho,” alisema.

Alisema watu wazima kuanzia miaka 45 wanashambuliwa na ugonjwa huo kwa asilimia 80 na ikitokea akaupata mtoto basi huwa ameambukizwa na mama yake akiwa tumboni

“Iwapo tutapata mashine za kisasa kama za Wajapan ukiachilia faida ya upasuaji bila kidonda, itatuongezea idadi ya wagonjwa tutakaotibia kwa siku.

“Badala ya kutumia dakika 15 kwa upasuaji mmoja, tutatumia dakika tano pekee, hivyo kwa siku tutakuwa na uwezo wa kutibia wagonjwa wanane hadi 10,” alisema.

Alisema wamekuwa wakishirikiana na Japan kwa miaka 11 kwa kuleta wataalamu kwa ajili ya upasuaji.

Akizungumzia huduma hiyo, Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida alisema anafurahishwa na ushirikiano wa nchi hiyo na Tanzania hususani katika suala la afya.

Alisema wamekuwa wakishirikiana katika mambo mengi ikiwamo kutoa utaalamu.

“Nimeridhishwa na ujio wa wataalamu hawa, naamini mbali na kutoa huduma kwa wagonjwa, pia watawaachia wenzao utaalamu, ” alisema Balozi Yoshida.