Wajichimbia kujadili sheria ya ndoa
Muktasari:
- Viongozi wa dini waona umuhimu kufanyika mabadiliko umri wa msichana kuolewa.
Dar es Salaam. Viongozi wa dini wameweka msimamo kuhusu ndoa za utotoni, wakionyesha nia ya kuunga mkono marekebisho ya sheria ya ndoa.
Wamesisitiza mtoto ataolewa kwa jambo lenye masilahi kwa wakati huo na hekima ya mzazi wake.
Viongozi hao wametoa msimamo huo wakati takwimu zikionyesha wasichana wawili kati ya watano wanaolewa katika umri chini ya miaka 18, wengi wakitajwa ni wale wa kutoka familia masikini.
Viongozi wa dini wametoa msimamo leo Jumanne, Desemba 5, 2023 wakati wa majadiliano ya pamoja kati yao, wanasheria, watetezi wa haki za binadamu na wadau wengine mbalimbali.
Akizungumza katika mkutano huo, Padri Florence Rutaiwa wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), amesema suala hilo kwa sasa linaangaliwa katika mustakabali wa mabadiliko ya kitabia na wanadamu, hivyo viongozi wa dini wanaunga mkono.
Amesema awali, walisimamia sheria ya Kirumi iliyoruhusu msichana wa miaka 12 kuolewa na mvulana wa miaka 14 kuoa, kabla haijarekebishwa mwaka 1983 na kuwa miaka 14 kwa msichana na 16 kwa mvulana.
"Zamani lishe ilikuwa bora, umri huo ulitosha kuoa na kuolewa, lakini ukisoma sheria ya kanisa ya mwaka 1071 aya ya pili, inasema endapo hakuna sababu ya lazima na endapo ina msukumo mkubwa sana, mtu yeyote asishuhudie ndoa itakayokwenda kinyume cha sheria za nchi pasipo ruhusa ya askofu.
"Lakini sasa chini ya miaka 18 bado ni mtoto na sisi lazima twende na utaratibu uliowekwa na nchi, hivyo tunasubiri sheria. Ukisoma sheria ya kanisa inasema mtu yeyote asifungishe ndoa inayopingana na sheria ya nchi," amesema.
Sheikh wa Wilaya ya Ubungo, Maulid Salim Kidebe amesema mtoto chini ya umri wa miaka 18 ataolewa kwa kuangalia jambo lenye masilahi kwa mtoto kwa wakati huo na hekima ya mzazi wake.
"Tutaangalia lipi lina masilahi kwa mtoto na hii ni msimamo wa dini ya Kiislamu kwa kuwa sasa hivi mtoto wa miaka 15 tayari ni mtu mzima na hata ukiangalia maeneo mengine tayari wanafanya matukio na wengine wanapewa vidonge vya uzazi wa mpango," amesema.
Sheikh Kidebe amesema Baraza la Ulamaa limeona kwa sasa suala hilo litabaki kwa masilahi ya mtoto na hekima ya mzazi.
Katika mjadala huo, kuliibuka hoja ya ukinzani wa sheria kuhusu mtoto.
Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Msichana Initiative, Rebecca Gyumi amesema mikataba ya sheria ya kazi na ile inayotambua mpiga kura, inamtafsiri mtu chini ya miaka 18 kuwa bado ni mtoto.
Amesema suala hilo limekuwa likileta utata hasa kwa binti wa chini ya umri huo anayesoma, sheria hiyo humsaidia ikilinganishwa na yule aliye nje ya mfumo wa shule, hivyo haileti usawa.
"Mkwamo uliopo katika mabadiliko ya sheria ya ndoa hasa katika vifungu vya 13 na 17 vinavyoruhusu ndoa chini ya miaka 15, lakini kutokana na kikao cha leo labda tunatumia dini na mila kama kikwazo, lakini leo hapa ushahidi tunaona viongozi hawa si kikwazo," amesema Rebecca.
Amesema, "Serikali isitumie dini kama kikwazo, viongozi hawa wanaonekana wana utayari na nia ya kuona sheria hii inatoka kwenye mkwamo uliopo."
Kuhusu hilo, Sheikh Kidebe amesema licha ya kwamba damu inachemka katika umri wa balehe, kuwaozesha wasichana si kutatua tatizo bali ni kuongeza zaidi matatizo kwa kuleta vifo vitokanavyo na mimba za utotoni, unyanyasaji wa kijinsia na mengineyo.
Ametoa mfano wa nchi zilizopitisha sheria ya mtoto kutoingia kwenye ndoa chini ya umri wa miaka 18 zikiwamo Malawi, Falme za Kiarabu, Zimbabwe na Bangladesh.
Mkuu wa dawati la jinsia Kanda ya Dar es Salaam, Leah Mbunda amesema ndoa nyingi ambazo hufikia hatua ya kuvunjika au wanandoa kuwa na migogoro ya mara kwa mara unakuta binti aliozwa akiwa na umri mdogo.
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Agnes Mangala amesema ni vyema sheria inayozuia ndoa hizo ikapitishwa.
Amesema lengo ni kusaidia vijana, hivyo wataalamu wasikilizwe.
Mwaka 2016 Gyumi alishinda kesi aliyofungua mahakamani kupinga sheria ya ndoa ya mwaka 2017. Serikali ilikata rufaa ikisema sheria ilitungwa ili kutumika na makundi mbalimbali yakiwamo ya kidini, kimila na kuwa mwaka 1971 walipoitunga waliweka mazingira watoto wa kike kupewa upendeleo.
Mwaka 2019 Serikali ilipewa muda wa mwaka mmoja mpaka 2020 kuifanyia marekebisho sheria hiyo.
Mwaka 2021 ulipelekwa muswada bungeni kuweka umri wa kuolewa kuwa miaka 18, hata hivyo baadaye Serikali ilielekezwa na Bunge kurudi kwa umma kupata maoni.