Wakamatwa kwa kuazimisha silaha kwa watuhumiwa wa ujambazi

Friday May 20 2022
ujambazi pc
By Stephano Simbeye

Songwe: Jeshi la Polisi mkoani Songwe linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kuazimisha silaha wanazomiliki kihalali kwa watu wanaotuhumiwa kwa matukio ya ujambazi.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Jannet Magomi amewaambia waandishi habari leo Ijumaa Mei 20, 2022 kuwa, jeshi hilo limekuwa katika msako kwa ajili ya kudhibiti uhalifu na kufanikiwa kumkamata mkazi wa kijiji cha Ikana wilayani Momba, Edward Sikalengo akiwa na risasi.

Magomi amesema baada ya Sikalengo kuwataja jeshi la polisi lilifanikiwa kuwakamata, Izukanji Sikalengo (60), na Izukanji Siwiti (60) wote wakazi wa kijiji cha Machindo kata ya Kapele wilayani Momba.

Amesema katika operasheni hiyo pia jeshi hilo limefanikiwa kukamata pikipiki saba katika wilaya za Mbozi na Songwe ambazo zinadaiwa kuporwa na nyingine kuibiwa baada ya nyumba kuvunjwa.

Aidha Kamanda Magomi amesema katika msako huo pia jeshi hilo limefanikiwa kukamata mali kadhaa za wizi ikiwemo nyara za serikali, runinga, magodoro na bangi

Advertisement