Wakamatwa kwa kuua twiga ili wakauze nyama

Watuhumiwa wa ujangili wa Twiga, Masiali Kipara na Paulo Richard wakiwa chini ya Ulinzi wa askari wa Wanyamapori baada ya kukamatwa eneo la Jumuiya ya hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge Wilaya ya Babati

Babati. Wakazi wawili wa Kijiji cha Minjingu, Wilaya ya Babati Mkoa wa Arusha, Masiali Lais Kipara (19) na Paulo Richard (23) wamekatwa na Twiga mdogo, wakiwa tayari wamemuua ili kufanya biashara ya kuuza nyama.

Biashara ya nyama ya Twiga, imeanza kushamiri katika maeneo ya Mji wa Magugu na Babati  Mkoa wa Manyara kutokana na maeneo hayo, kuwa ni mapito ya wanyama kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na Hifadhi ya Taifa ya Manyara.

Watuhumiwa hao, walikamatwa katika eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge (Burunge WMA) na askari wa wanyamapori, Askari wa Jumuiya ya  Hifadhi ya Wanyamapori ya Burunge kwa kushirikiana na Askari wa Taasisi ya Chemchem ambayo imewekeza katika eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, George  Katabazi akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 22, 2023 amesema, twiga huyo mdogo mwenye kilo 54.5  mwenye thamani ya Sh35.1 milioni na  alikutwa tayari ameuawa.

Akizungumza na mwananchi askari wa wanyamapori ambaye aliongoza operesheni kukamamata watuhumiwa hao, Samweli Bayo akiwa doria na askari wenzake wa Burunge WMA na Chemchem, waliwakuta watuhumiwa na nyama hiyo, wakijipanga kuanza kuchuna ili wakauze.

Bayo amesema tukio hilo lilitokea Februari 14, saa 11 jioni na  walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao, wakiwa porini na watuhumiwa wengine wawili walikimbia.

Afisa Idara ya kupambana na ujangili wa taasisi ya Chemchem association ambayo imewekeza utalii wa picha na hoteli katika eneo hilo, Erick Nyman amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao ni jitihada za ulinzi shirikishi.

Amesema wamekuwa wakifanya doria  ya pamoja baina ya askari wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori (TAWA), Askari wa wanyamapori Wilaya ya Babati, Askari wa Chemchem na Askari wa Burunge WMA.

Nyman amesema taasisi hiyo kwa mwaka imekuwa ikitumia zaidi ya Sh400 milioni katika harakati za kupambana na ujangili katika eneo hilo la Burunge WMA  kutokana na kushamiri matukio ya ujangili ukiwepo wa Twiga na wanyama wengine kwa ajili ya kitoweo.