Wakazi 36,000 kunufaika na mradi wa maji, watakiwa kuutunza
Muktasari:
Wananchi zaidi ya 36,000 watakaonufaika na mradi wa maji ya bomba katika Kata za Katwe, Bagwe na Bupandwa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wametakiwa kutunza miundombinu ya mradi huo ili wanufaike na kupata huduma bora.
Buchosa. Wananchi zaidi ya 36,000 watakaonufaika na mradi wa maji ya bomba katika Kata za Katwe, Bagwe na Bupandwa Halmashauri ya Buchosa wilayani Sengerema wametakiwa kutunza miundombinu ya mradi huo ili wanufaike na kupata huduma bora.
Akitoa wito huo Novemba 10, 2023 wakati wa ziara yake ya kutatua kero na kukagua miradi ya maendeeleo katika halmashauri hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amewataka wakazi hao kuutunza vyema utakapokamilika mwaka 2024.
Huku akiipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Sengerema inayotekeleza mradi huo kwa gharama ya Sh7.1 bilioni amesema Serikali inatoa fedha nyingi ili kutatua changamoto ya ukosefu wa maji kwa wananchi.
“Ruwasa mnafanya kazi nzuri endeleeni kutekeleza miradi ya maji wananchi wanataka maji na siyo maneno, Serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji...tuendelee kuwasaidia wananchi wapate maji,” amesema Makalla
Nao wananchi wa Kata ya Katwe akiwemo, Asteria Makama wameishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo utakaowasaidia kupata maji safi na salama.
Awali akisoma taarifa kwa Makalla, Kaimu Meneja wa Ruwasa wilayani Sengerema, Elisha Sembo amesema mradi huo utakuwa na matanki matatu yakuhifadhi maji ambapo tanki moja litakuwa na lita 6,000 na mawili yatakuwa na lita 3,000 kila moja.
Sembo amesema pia utakuwa na vituo zaidi ya 100 vya kuchotea maji akidai licha ya kuhudumia wakazi 36,000 kwa sasa mradi huo unauwezo wa kuhudumia wakazi 88,000.
Katika ziara yake kwenye halmashauri ya Buchosa, Makalla amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo kikiwemo chuo cha Veta, jengo la wagonjwa wa dharula Hospitari ya Buchosa na mradi wa maji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buchosa, Benson Mihayo amesema licha ya kuwepo utekelezaji wa miradi, Serikali imetoa zaidi ya Sh2 bilioni kutekeleza miradi ya elimu na afya kwenye halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Sengerema, Marco Mkaoye ametoa angalizo mradi huo utakapo kamilika wahusika wahakikishe wanaweka bei rafiki ili wananchi waweze kumudu kuonganisha huduma hiyo majumbani mwao.