Wakazi Kibaha walilia maji, wamtumia ujumbe Rais Samia

Muktasari:

  • Wakazi wa Mtaa wa Mchikichini, Kata ya Mkuza, Halmahauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia uwezekano wa kuwasaidia ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji wanayodai kuikosa kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

  


Kibaha. Wakazi wa Mtaa wa Mchikichini, Kata ya Mkuza, Halmahauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia uwezekano wa kuwasaidia ili kuondokana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji wanayodai kuikosa kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Wakizungumza leo Alhamisi, Septemba 15, 2022 wamesema wamefikia hatua hiyo ya kuomba msaada kwa mkuu wa nchi baada ya kupeleka kilio chao kwa uongozi wa mamlaka ya maji mkoani humo mara kadhaa lakini hakuna utatuzi wowote huku wakiendelea kutaabika.

"Tuna zaidi ya miezi mitatu sasa hatuna huduma ya maji, hatujui tatizo nini maisha yanakuwa magumu bila maji," amesema Janeth Adamu.

Amesema hivi sasa wanalazimika kununua maji Sh1000 kwa ndoo yenye ujazo wa lita 20 jambo ambalo linawauwia ugumu ukilinganisha na uchumi wa sasa.

Joyce Mbwambo, mkazi wa mtaa huo amesema anashagazwa na Mamlaka ya Maji Mjini humo kutoshughulikia kero yao huku wakiendelea kupata shida ya maji.

"Ukitoka hapa wenzetu mtaa wa pili wanapata huduma ya maji lakini sisi hatupati maji na tumepiga kelele sana kwao," amesema

Naye Edwin Lomanyika amesema hivi sasa wanahofua usalama wa afya zao kwani maji wanayotumia ni ya chumvi yanayochotwa kwenye kisima.

Akizungumzia changamoto hiyo, Meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), Mkoa wa Kibaha Alpha Ambokile amesema atalifanyia kazi suala hilo.