Wakili aliyetetea ujira wa mawakili wa kujitegemea Tanzania afariki

Wakili aliyetetea ujira wa mawakili wa kujitegemea Tanzania afariki

Moshi. Wakili mwandamizi nchini Tanzania, Lord Ng’uni ambaye mwanzoni mwa miaka ya 90 aliweka msingi wa mawakili wa kujitegemea kulipwa vizuri amefariki dunia.

Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Januari 26, 2021 na Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) mkoa Kilimanjaro inaeleza kuwa wakili huyo aliyeandikishwa kwa namba 383 mwaka 1978 alifariki dunia jana Januari 25, 2021  katika hospitali ya rufaa ya KCMC mjini Moshi.

Mwenyekiti wa TLS mkoa Kilimanjaro, David Shillatu, amesema Ng’uni ambaye alikuwa pia mkuu wa wabantu na ubantu duniani, alifariki dunia  wakati akitibiwa na kwamba  taratibu za mazishi zinafanyika kwa kushirikiana na familia yake.

“Tutaendelea kumkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sheria nchini,” amesema Shillatu.

Shillatu amesema atakumbukwa kupitia uamuzi wa mahakama ya rufaa mwaka 2002 iliyopandisha malipo ya mawakili wa kujitegemea kutoka Sh500 hadi Sh100,000.

“Huu ulikuwa ni ushindi mkubwa kwa mawakili wa kujitegemea na kwa kweli yalikuwa ni matunda mazuri ya wakili huyu mwandamizi kwa sasa kwa taaluma nzima ya mawakili wa kujitegemea nchini,” amesema.


Kwanini mawakili watamkumbuka

Mwaka 1993,  Ng’uni alipangiwa kesi tofauti sita za jinai kuwatetea  washtakiwa wasio na mawakili na wakati huo ujira wa juu kwa wakili ukiwa Sh500 kwa kesi moja, malipo ambayo aliyapinga.

Kutokana na kitendo hicho, Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Arusha alimsimamisha kufanya kazi ya uwakili wa kujitegemea, alipinga na kukata rufaa  mahakama kuu ya Tanzania na kushinda.

Hata hivyo, Jaji mfawidhi na mwanasheria mkuu wa Serikali (AG) wakati huo walikata rufaa iliyopewa nambari 45 ya 1998 ambapo kesi hiyo ilipangiwa majaji watatu kwa kuwa msingi wake ulikuwa unagusa katiba.

Majaji hao ni;  Jaji Lewis Makame, Jaji Agustino Ramadhan na Jaji Kahwa Lugakingira waliokubaliana na  hoja za Lord Ng’uni kwamba malipo ya Sh500 aliyotakiwa kulipwa kwa kila kesi yalikuwa na madogo.