Wakili aliyeteuliwa kuwa jaji akwamisha kesi ya Gugai na wenzake

Wakili aliyeteuliwa kuwa jaji akwamisha kesi ya Gugai na wenzake

Muktasari:

  • Kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato inayomkabili aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake wawili imekwama kuendelea katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Dar es Salaam. Kesi ya utakatishaji fedha na kumiliki mali zilizozidi kipato inayomkabili aliyekuwa mhasibu mkuu wa Takukuru, Godfrey Gugai na wenzake wawili imekwama kuendelea katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Kukwama huko kunatokana na wakili aliyekuwa anaendesha shauri hilo, Awamu Mbangwa kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Mbangwa ambaye alikuwa wakili wa Serikali mwandamizi  aliapishwa jana Ikulu Dar es Salaam na wenzake 27.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Mei 18, 2021 na wakili kutoka Takukuru, Ipyana Mwakatobe wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuendelea na ushahidi wa upande wa mashtaka.

Mwakatobe amedai mbele ya  hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Thomas Simba kuwa Mbangwa sasa ni jaji na kuomba kesi hiyo ipangiwe tarehe nyingine.

"Kesi hii ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji upande wa mashitaka lakini  aliyekuwa wakili mwenzangu, Awamu Mbagwa ameteuliwa kuwa jaji, hivyo naomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji lakini pia kulipitia jalada husika kwa sababu kesi hii ilikuwa inaendeshwa na wakili mwingine" alidai.


Mwakatobe baada ya kueleza hayo, Hakimu Simba, amesema kesi hiyo lazima iendelee hivyo upande wa mashtaka wajipange kwa ajili ya tarehe ijayo na kuahirisha kesi hadi Mei 31 na Juni 2, 2021.

Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka ya kutakatisha fedha yanayowakabili kutokuwa na dhamana.

Mpaka sasa mashahidi 40 wa upande wa mashitaka wameshatoa ushahidi wao.

Mbali na Gugai, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni wafanyabiashara George Makaranga na Leonard Aloys wanaokabiliwa na mashtaka 40.

Kati ya mashtaka 40 yanayowakabili, 19 ni ya  kughushi, 20 utakatishaji fedha na moja ni kumiliki mali zilizozidi kipato halali.

Shtaka la kumiliki mali kinyume na kipato chake linamkabili Gugai peke yake akidaiwa kulitenda kati ya Januari 2005 na Desemba 2015.

Inadaiwa Gugai, akiwa jijini Dar es Salaam kama mwajiriwa wa Takukuru alikuwa akimiliki mali za zaidi ya Sh3.6 bilioni ambazo hazilingani na kipato chake cha awali na cha sasa na kushindwa kuzitolea maelezo.