Wakili Marenga: Uhuru wa uhariri unaingiliwa

Muktasari:

Makamu Mwenyekiti wa MISA – TAN na wakili wa kujitegemea, James Marenga ameiomba Serikali kukifuta kifungu cha sheria ya huduma za habari kinaingilia uhuru wa mhariri wa habari kuamua habari ya kuchapisha au kutangaza.

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa MISA – TAN na wakili wa kujitegemea, James Marenga ameiomba Serikali kukifuta kifungu cha sheria ya huduma za habari kinaingilia uhuru wa mhariri wa habari kuamua habari ya kuchapisha au kutangaza.

Marenga ametoa ombi hilo leo kwenye semina na wanahabari iliyolenga kuangalia kasoro zilizomo sheria hiyo ya mwaka 2016.

Marenga amesema hatua ya mhariri wa chombo cha habari kuelekezwa na Serikali taarifa za kuchapisha, kama ilivyolekezwa na kifungu cha cha 7 (2) (b) cha sheria hiyo, inaingilia moja kwa moja uhuru wa mhariri katika kutoa ama kuchapisha habari.

“Kifungu cha 7 (2) (b) (iv) b cha Sheria ya Huduma za Habari, kinatoa maelekezo kwa vyombo vya habari binafsi kuchapisha habari zenye umuhimu kwa taifa kwa maelekezo ya Serikali.

Kifungu hiki cha Sheria kinaingilia uhuru wa uhariri na hasa kwenye vyombo vya habari vya binafsi. Kifungu hiki kidogo hakiwezi kufanyiwa marekebisho, tunapendekeza kifutwe,” amesema.

Amesema, mapendekezo yanakusudia kuwezesha maamuzi ya kihariri kuzingatia vigezo vya taaluma bila kuathiriwa na maamrisho yasiyo ya kitaaluma. Uhuru wa uhariri utalindwa.

Akifafanua zaidi amesema, kifungu cha 7 (3), (a), (b), (c), (f), (g), (h), (i) na (j) vya Sheria hiyo, vinatoa udhibiti wa aina fulani ya habari ama maudhui.

“Mamlaka hii ya kisheria inatoa mwanya kwa serikali kudhibiti taarifa zinazotolewa na vyombo binafsi vya habari.

“Kifungu hiki na vifungu vyake vidogo vinakiuka uhuru wa wa kujieleza bila ya kuwa na sababu za msingi. Hii pia ni kwa mujibu wa maamuzi ya Mahakama ya Haki ya Afrika ya Mashariki (EACJ).

Amesema, tunapendekeza kifungu hiki na vifungu vyake vidogo vifutwe kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki. (EACJ),” amesema Wakili Marenga.

Kwenye semina hiyo Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) amesema, wameungana kwa pamoja katika kuhakikisha wanaweka mazingira rafiki kwa wanahabari kufanya kazi zao.

“Kuna sheria nyingi zilizowekwa na kulenga waandishi ama kushambulia tasnia, kwa tumeungana kwa pamoja kuhakikisha sheria hizo zinaondolewa makali yanayoumiuza wanahabari.

“Ni bahati nzuri sasa serikali nayo imeliona hili, mwelekeo wetu ua matumaini lakini tunapaswa kuendelea pamoja mpaka tunafikia lengo,” amesema Balile.