Wakimbizi wa Burundi wapewa hadi Desemba 31 kurudi kwao
Muktasari:
- Serikali ya Tanzania na Burundi zinaendelea kuwahamasisha wakimbizi kutoka nchini Burundi wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu na Nduta mkoani Kigoma, kuendelea kujiandikisha na kurejea nyumbani kwa hiari hadi Desemba 2024.
Kigoma. Serikali ya Tanzania imesema haitaongeza muda wa uhamasishaji wakimbizi kutoka nchini Burundi waishio kambi ya Nyarugusu na Nduta zilizopo mkoani Kigoma, kurudi nchini kwao kwa hiari ifikapo Januari, mosi 2025.
Hatua hiyo imekuja mara baada ya makubaliano ya pande tatu, Serikali ya Tanzania, Burundi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), kukubaliana kutoa kipindi cha miezi 12 cha ongezeko la muda wa kuwahamasisha kurejea nchini kwao kwa hiari kuanzia Januari hadi Desemba 2024.
Akizungumza leo mjini Kigoma, wakati wa kufunga kikao cha majadiliano cha siku tatu cha pande mbili kati ya Serikali ya Tanzania na serikali ya Burundi kilichokuwa kinajadili masuala mbalimbali yanayohusiana na wakimbizi, Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni amesema hatua hiyo imefikiwa mara baada ya kujiridhisha kuwepo na amani na kuendelea kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo nchini Burundi.
“Kwa sasa tupo katika kipindi cha kuwahamasisha kurejea nchini kwao kwa hiari hadi Desemba 31, 2024 baada ya hapo mpango huo usipokamilika, wakimbizi hao watakuwa wamepoteza hadhi yao ya ukimbizi hivyo hatua itakayofuata ni kuwahoji mmoja mmoja na kujua sababu za kwa nini waendelee kubaki nchini pamoja na kuwepo kwa amani na utulivu nchini mwao,” amesema Masauni
Masauni amesema hatua ya kuwahamasisha kurejea nchini kwao kwa hiari, inaenda sambamba na utekelezaji wa makubaliano yao pamoja na kuzingatia sheria zote zikiwemo za ndani ya Tanzania na kimataifa, ili kuhakikisha wakimbizi hao wanapata suluhisho la kudumu la kurejea nchini kwao.
Katibu Mkuu Wizara ya Ndani na Maendeleo ya Jamii na Usalama wa Raia nchini Burundi, Theofile Ndarufatiye amesema tangu mwaka 2017 hadi kufikia mwaka 2024 jumla ya wakimbizi 1,070,607 wamerejea nchini humo.
Amesema kwa kipindi cha Januari hadi Mei 2024 pekee jumla ya wakimbizi 5,709 wamerejea nchini Burundi, huku zaidi ya wakimbizi 100,000 wakiwa bado wapo katika kambi ya Nduta na Nyarugusu.
“Tunawashukuru Watanzania kuendelea kutoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka nchini kwetu Burundi na niendelee kuwatia moyo Warundi kuendelea kujiandikisha kwa wingi ili kuweza kurejea nyumbani kwa hiari kwani baada ya kujiandikisha utapatiwa fedha za kujikimu ambapo ni dola za kimarekani 200, makazi, vifaa vya ujenzi pamoja na huduma nyingine za kijamii,” amesema Ndarufatiye
Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema hali ya urejeaji wa wakimbizi nchini kwao bado inasuasua pamoja na hali ya utulivu na amani kurejea nchini Burundi, na kwamba wao kama serikali kwa kushirikiana na serikali ya Burundi inaendelea na hatua za kuwahamasisha kurejea kwa hiari.