Wakimbizi waliopo Tanzania wagoma kurejea Burundi
Muktasari:
- Asilimia 95 ya wakimbizi wa kambi ya Nyarugusu, wilaya Kasulu, Mkoa wa Kigoma nchini Tanzania hawako tayari kurejea nchini kwao kwasababu mbalimbali ikiwemo za kiusalama.
Kasulu. Asilimia 95 ya wakimbizi wa kambi ya Nyarugusu, wilaya Kasulu, Mkoa wa Kigoma nchini Tanzania hawako tayari kurejea nchini kwao kwasababu mbalimbali ikiwemo za kiusalama.
Akizungumza leo Jumatano, Novemba 30, 2022 ndani ya kambi ya Nyarugusu, wakati akitoa taarifa ya kambi hiyo kwa viongozi kutoka Burundi na Serikali ya Tanzania, Mkuu wa kambi hiyo, Siasa Manjenje amesema hadi kufikia Novemba 28, 2022 idadi ya wakimbizi na waomba hifadhi waliopo kambini ni 129,870.
Amesema Julai, 2022, Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR), waliwahoji wakimbizi wa Burundi ili kujua kwanini hawarejei nyumbani.
Amesema katika kambi ya wakimbizi Nyarugusu, asilimia 95 walionesha nia ya kutokurejea nyumbani kutokana na sababu ya uhaba wa ardhi na makazi, ukosefu wa shughuli za kujikimu, hofu ya usalama na ukosefu wa huduma bora za kijamii.
“Kwa mwaka huu tangu Januari hadi Novemba, jumla ya wakimbizi 1,602 kutoka kambi ya Nyarugusu ndio walirejea nchini Burundi, wastani wa urejeaji katika kambi hiyo kwa wiki ni watu 50 hadi 60 kati ya watu 1400 waliopaswa kurejea kwa wiki,” amesema Manjenje.
Naye Naibu Waziri wa Mambo ya ndani wa Burundi, Nibona Bonansize Celestin amesema kwa sasa hakuna kitisho chochote cha kuwazuia wakimbizi kurejea nchini kwao na kwenda kuishi kama zamani kwani amani na usalama vimetawala.
Inspekta Jenerali wa Polisi wa Burundi, Ndihokubwayo Isidore amewahakikishia wakimbizi uwepo wa usalama wa kutosha ukilinganisha na wakati walipokimbia.
Barubike Marie ni raia wa Burundi aliyewahi kuwa mkimbizi na sasa amerejea nchini mwake anashuhudia Burundi ina amani na kuwahimiza waliosalia kambini kuepuka uvumi na waamue kurejea.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andebgenye amesema suluhisho la ukimbizi ni kurejea nyumbani na kwamba ipo fursa ya Warundi kuingia Tanzania kwa shughuli za kiuchumi badala ya ukimbizi.
Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR limeweka mpango maalumu wa kuwahamasisha wakimbizi wa Burundi kurejea nchini mwao, ambapo mpango huo uliopewa jina la “njoo utoe ushuhuda” unahusisha raia wa Burundi waliokuwa wakimbizi nchini Tanzania kuja kukutana na wakimbizi makambini na kuwaelezea uhalisia wa usalama na amani nchini mwao.
Katika mpango huo jumla ya Warundi 10 wakiwemo vijana wanawake na wazee wameongozana na viongozi wa UNHCR Burundi, viongozi wa Serikali ya Burundi na wanaungana na viongozi wa Serikali ya Tanzania kutembelea kambi ya wakimbizi.