Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakosa makazi nyumba 120 zikiezuliwa na upepo Zanzibar

Mwonekano wa baadhi ya nyumba zilizoezuliwa na upepo mkali uliotokea hivi karibuni katika Mkoa wa Kaskazini Unguja ambapo nyumba 124 na misikiti miwili viliezuliwa na kuwaacha wananchi bila makazi. Picha na Jesse Mikofu

Unguja. Baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wamekosa makazi baada ya nyumba 124 na misikiti miwili kuezuliwa na upepo mkali.

Mbali na nyumba hizo na msikiti, upepo huo uliotokea Aprili 7, pia umeathiri mazao na miti katika shehia sita za mkoa huo.

Akizungumza alipozitembelea familia zilizoathiriwa na upepo huo, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla mbali na kuwapa pole, alisema Serikali kwa kushirikiana na wadau watahakikisha wanarudi katika makazi yao ya awali kwa kipindi kifupi.

“Serikali ipo pamoja nanyi, kikubwa tuwe na subra katika kipindi hiki cha mtihani huu. Tutaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha hali inarejea kama kawaida,” alisema.

Aliwapongeza wananchi waliowahifadhi waathirika hao katika makazi yao na kueleza kuwa kitendo hicho kinaonyesha umoja na mshikamano katika jamii.

Hemed pia aliwashukuru wadau mbali mbali wa maendeleo waliotoa kusaidia wa vifaa mbalimbali vya ujenzi kwa wananchi hao pamoja na kuisaidia Serikali katika kuwafariji waathirika hao.

Pia, Hemed alikabidhi mabati 80 kwa ujenzi wa msikiti wa Shehia ya Kigongoni na kupokea mabati 50 yaliyotolewa na mwananchi mzalendo, Makame Simai kwa ajili ya kuwafariji waathirika hao.

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa huo, Ayoub Muhamed Mahmoud alisema ni vema wananchi kufuata ushauri wa kitaalamu wakati wa ujenzi wa nyumba zao, ili kuepukana na madhara mbalimbali.

Baadhi ya wananchi walioathirika na upepo huo akiwemo Abubakari Khalid alimshukuru Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwenda kuwafariji katika kipindi hiki kigumu na kueleza hatua hiyo inaonyesha namna Serikali inavyowajali wananchi wake.