Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima Arumeru wageukia pareto

Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda (kushoto) akielekezwa na mtaalamu kutoka kampuni ya Pareto Tanzania (PCT) Gerald Joseph jinsi ya kung'oa Miche ya Pareto kutoka kwenye kitalu kwa ajili ya kugawa kwa wakulima awamu ya kwanza, wakati wa  uzinduzi wa ugawa miche hiyo bure kwa wakulima. Picha na Bertha Ismail 

Muktasari:

  • Wakulima hao walipatiwa miche bure, utaalamu wa namna ya kuanza kuandaa shamba hadi kustawisha sambamba na kuanzishiwa vituo vya ununuzi wa pareto inayotumika kutengeneza viuatilifu vya kuulia wadudu kwenye mimea mingine.

Arusha. Wakulima katika wilaya ya Arumeru mkoani hapa wanatarajia kuanza kunufaika na kilimo cha pareto baada ya kuanza kugawiwa bure miche ya zao hilo, ili kuwakwamua kiuchumi na kuachana na kilimo cha bangi.

Shughuli hiyo inakwenda sambamba na kupewa ujuzi wa namna ya kuanza kuandaa shamba hadi kustawisha sambamba na kuanzishiwa vituo vya ununuzi wa pareto inayotumika kutengeneza viuatilifu vya kuulia wadudu kwenye mimea mingine.

Akizungumza leo Februari 14, 2024 wakati wa uzinduzi wa ugawaji miche kwa wakulima, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda amesema ameamua kuwekeza nguvu katika kuhakikisha anatokomeza kilimo cha bangi wilayani humo kutokana na kuaibishwa mbele ya Rais Samia Suluhu, Juni 25, 2023.

“Hakuna siku niliona aibu kama ile siku ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya duniani Juni 25, 2023 mbele ya Rais wangu, baada ya eneo langu la kazi (wilaya ya Arumeru) kutajwa kuongoza kitaifa kwa kilimo cha bangi, hakika niliona aibu sana,” amesema Kaganda.

Amesema baada ya hapo walianza utafiti wa mazao mbadala yanayostawi katika eneo hilo na kugundua kuwa pareto ni mojawapo, hivyo wakaanza utaratibu wa kuwasaidia wakulima kugeukia kilimo hicho.

“Tulianza kwa kutoa elimu kwa wakulima hasa huku Kisimiri juu wanaolima sana bangi kwa kushirikiana na wadau wakiwemo kampuni ya Pareto Tanzania (PCT), ambapo pia walianzisha vitalu vya miche na leo tumekuja kuzindua ugawaji miche kwa wakulima,” amesema.

Kaganda amewataka wananchi wa Arumeru hasa Kisimiri juu wanaoanza kupatiwa miche hiyo waitunze kwa manufaa yao ya kiuchumi.

“Oneni umuhimu wa kutunza miche hii na kujikita kwenye kilimo hiki chenye faida kubwa na halali isiyo na usumbufu wala gharama za mbolea na sumu za wadudu, kwa maendeleo yenu wenyewe na usalama wa afya za watoto wenu na Taifa kwa ujumla” amesema Kaganda.

Awali, wananchi wa Kisimiri juu walisema ili Serikali ifanikiwe kutokomeza kilimo cha bangi katika eneo hilo,  lazima iboreshe miundombinu ya umwagiliaji na barabara ya kufikika kwa ajili ya kusaidia mazao mengine kustawishwa na kupelekwa sokoni.

“Kilimo cha pareto tumepokea kwa mikono miwili, lakini hatuwezi kuishi kwa pareto tu, Serikali ituletee maji ili tulime na mbogamboga na  mazao ya chakula kama mahindi na maharage kwa umwagiliaji, pia watuchongee barabara isaidie kusafirisha mazao yetu hadi kwenye masoko,” amesema Martha Mollel.

Mwakilishi wa kampuni ya PCT wanaotekeleza mradi huo wa kuhamasisha kilimo cha pareto nchini, Gerald Joseph amesema wameandaa miche kwenye vitalu inayotosha kuoteshwa kwenye mashamba ya zaidi ya ekari 300 kwa awamu ya kwanza.

“Tumeotesha miche kwenye ekari sita inayotosha  kuhamishiwa kwenye mashamba ya ekari zaidi ya 300 kwa awamu ya kwanza, na baadaye tutavuna tena zingine hadi kukamilisha mzunguko wa wananchi wote,”amesema.

Amesema kila kijiji kinaandikisha wananchi wenye mashamba na uhitaji wa miche hiyo ambapo wataanza kugaiwa bure,  na baadaye watanunua mavuno kwa bei elekezi ya Serikali ya Sh3,500 itakayowainua wananchi hao kiuchumi.

Amesema zao hilo linalostawi bila mbolea wala kushambuliwa na wadudu, litamwezesha mkulima kuanza kuvuna baada ya miezi mitatu ambapo kwa mchumo mmoja anaweza kupata zaidi ya kilo 50 hadi 60 kwa ekari moja.

“Mkulima wa Pareto anaweza kuanza kuvuna miezi mitatu baada ya kuotesha na atachuma kwa miaka mitatu mfululizo hadi minne, huku kiwango cha mavuno kikiongezeka hadi kilo 150 au 200 kwa ekari” amesema Gerald.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kisimiri juu, Mbayani Kuresoi amesema kuwa ameshaandikisha wanakijiji zaidi ya 240 walioonyesha nia ya kupokea miche hiyo kwa awamu ya kwanza, na tayari yamewapa wakulima 90.

Aidha Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo alisema kuwa kwa miezi sita kuanzia Januari hadi Juni 2023 walifanikiwa kuwakamata watu 16 kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya aina ya bangi katika eneo la Kisimiri juu.

“Mbali na kukamata watu, tuliteketeza magunia 953 ya bangi kavu na mashamba yenye ukubwa wa ekari 4,795” alisema Juni 25, 2023  kwenye siku ya kimataifa ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya.