Wakulima Manyara wanufaika na mikopo ya matrekta
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa kampuni ya PASS Leasing, Killo Lussewa (kushoto) baada ya kukabidhi mkopo wa matrekta 25. Picha na Joseph Lyimo
Muktasari:
- Wakulima 25 wa Mkoa wa Manyara, wamenufaika na mkopo wa matrekta 25 ya thamani ya Sh1.3 bilioni kwa lengo la kuboresha kilimo na kuongeza tija.
Babati. Wakulima 25 wa Mkoa wa Manyara, wamenufaika na mkopo wa matrekta 25 ya thamani ya Sh1.3 bilioni kwa lengo la kuboresha kilimo na kuongeza tija.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Charles Makongoro Nyerere ameyakabidhi kwa wakulima matrekta hayo yaliyotolewa na kampuni ya PASS Leasing Ltd.
"Nimpongeze mkulima mmoja Marco Mamoya ambaye amesema wakulima hawatasubiri maelekezo mara baada ya kupata matrekta ni kuelekea shambani," amesema Makongoro.
Mkuu wa wilaya ya Hanang' , Janeth Mayanja amesema anatarajia wakulima wa eneo hilo kunufaika kupitia kilimo cha mazao mbalimbali.
Mmoja kati ya wakulima waliochukua mkopo wa trekta yenye thamani ya Sh70 milioni John Marco amesema mkopo huo utarejeshwa ndani ya miezi mitatu baada ya kulipia asilimia 20.
Mkurugenzi wa kampuni ya PASS Leasing Ltd, Killo Lussewa amesema hadi hivi sasa kwenye mkoa huo wameshatoa mikopo ya zana za kilimo za thamani ya Sh1.3 bilioni.