Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakulima walalamikia mifugo kulishwa mazao yao mashambani

Sehemu ya shamba la ekari mbili inayodaiwa kuvamiwa na mifugo katika kata ya Mabogini wilayani Moshi.

Muktasari:

  • Julai 18, 2026, wananchi hao walikaa kikao na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sanya Line A, Thomas Ngonyani, kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Moshi. Wakulima katika Kitongoji cha Sanya Line A, Kijiji cha Mabogini, Moshi mkoani Kilimanjaro, wamelalamikia kukithiri kwa vitendo vya uvamizi wa mifugo katika mashamba yao, tatizo walilodai limeendelea kwa takribani miaka mitano.

Mbali na kuharibiwa kwa mazao, wakazi hao wanadai baadhi yao wamejeruhiwa wakati wakijaribu kuzuia mifugo kuingia mashambani, huku wakitilia shaka kuwepo kwa rushwa kwani wahusika hawachukuliwi hatua.

Julai 18, 2026, wananchi hao walikaa kikao na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sanya Line A, Thomas Ngonyani, kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.

Mwananchi ilifika katika eneo hilo linalodaiwa kutumiwa na wafugaji wanaotoka nje ya Wilaya ya Moshi kuhifadhi mifugo yao kabla ya kuipeleka malishoni na kukuta mashimo makubwa ardhini ambayo wananchi wanadai hutumika kama maboma ya mifugo, pamoja na mawe yaliyopangwa kama mafiga na mifuko iliyotelekezwa.

Wananchi hao, wanadai eneo hilo hutumika kama kituo cha muda cha wafugaji kabla ya mifugo kuingizwa kwenye mashamba ya wakulima.

Baadhi ya wananchi kitongoji cha Sanya Line A kata ya Mabogini wilaya Ya Moshi wakilalamikia adha ya mifugo kuvamia mashamba yao.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Ngonyani amesema migogoro kati ya wakulima na wafugaji imeendelea kwa muda mrefu licha ya juhudi mbalimbali za viongozi wa eneo hilo kuwasilisha malalamiko kwa mamlaka husika.

Amesema uchunguzi wao unaonyesha baadhi ya mifugo hiyo hutoka maeneo ya mbali kwa kuwa chapa zilizopo kwenye miili ya ng’ombe haziendani na zile zinazotambulika katika kijiji hicho.

Ngonyani, amedai baadhi ya wananchi wamekuwa wakiwapokea wafugaji hao na kuwasaidia kujenga maboma kwa maslahi binafsi, jambo linalochangia kuendelea kwa migogoro hiyo.

“Tulishakubaliana kuwa hakuna mfugaji anayepaswa kupokelewa bila taarifa kwa viongozi wa eneo husika. Hata hivyo, bado kuna wanaowapokea na kuwawezesha kuingia. Tumetoa taarifa kwa viongozi mbalimbali kuanzia ngazi ya kitongoji, kijiji, diwani na maofisa wa mifugo, lakini bado hatujaona suluhu ya kudumu,” amesema.

Ameongeza kuwa madai ya baadhi ya wafugaji kwamba wamekwishamalizana na viongozi wa juu yamekuwa yakichochea hisia miongoni mwa wananchi kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa, ingawa madai hayo hayajathibitishwa.

Mmoja wa wakulima wanaodai kuathirika na migogoro hiyo, Salim Raphael, amesema alijeruhiwa Julai 17, 2026 baada ya kukuta mifugo ikila mazao katika shamba lake.

“Nilipowauliza kwa nini mifugo yao ipo shambani kwangu, nilishambuliwa. Helmet niliyokuwa nimeivaa ilikatwa kwa mapanga na kupasuka. Pia nilipigwa mawe na kuumia mbavuni,” amedai Raphael.

Amesema tukio hilo lilisababisha uharibifu wa takribani ekari mbili za mahindi aliyokuwa ameyalima kwa gharama kubwa.

Naye, askari mstaafu, Thobias Chuwa, amesema miaka miwili iliyopita alijeruhiwa vibaya baada ya kuwafukuza ng’ombe waliokuwa wamevamia shamba lake.

“Nilipigwa hadi nikalazwa hospitalini nikiwa natapika damu. Hadi leo sijui hatima ya jalada la tukio hilo,” amesema.

Mbali na mashamba ya mazao, baadhi ya wakazi wanasema uvamizi huo umeathiri hata miradi mingine ya kiuchumi.

Marietta Mwongowi, amesema kisima chake cha kufugia samaki kimekuwa kikivamiwa na mifugo kwa wingi, hali ambayo imesababisha vifo vya samaki na hasara ya kifedha.

“Huu ni mwaka wa tano wa mateso haya. Tumekuwa tukitoa taarifa lakini bado hatujapata msaada wa kutosha,” amesema.

Kwa upande wake, Sergias Chuwa amesema tatizo hilo sasa limehamia hadi katika makazi ya wananchi, akidai mkewe aliwahi kushambuliwa na kujeruhiwa mguuni akiwa anakata majani karibu na nyumbani kwao.

Mwananchi mwingine, Carolina Profitilia, amesema wanawake wajane wanaotegemea kilimo ndio wanaoathirika zaidi kutokana na uvamizi wa mifugo.

“Tunalima kwa mikopo au kwa kukodisha mashamba. Unaporudi unakuta mazao yameharibiwa na mifugo. Hii inatuumiza kwa sababu ndiyo chanzo chetu kikuu cha chakula na kipato,” amesema.


DC afunguka

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Godfrey Mnzava, amesema Serikali inafahamu changamoto ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji katika eneo la Mabogini, hususan wakati wa kiangazi ambapo baadhi ya wafugaji kutoka maeneo mengine huingia na mifugo yao katika wilaya hiyo kutafuta malisho.

Amesema baadhi ya wafugaji hao hutoka Wilaya ya Simanjiro na maeneo mengine ya jirani, huku akisisitiza kuwa uhamishaji wa mifugo unapaswa kufanyika kwa kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kupata vibali vinavyotakiwa.

Mnzava, amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kudhibiti migogoro hiyo, ikiwemo kuunda kamati za usuluhishi zinazowashirikisha wakulima na wafugaji pamoja na kuweka utaratibu wa matumizi ya mabua ya mazao yanayonunuliwa na wafugaji baada ya mavuno.

Amesema mara nyingi changamoto hutokea pale mifugo inapoingizwa moja kwa moja mashambani baada ya kununuliwa mabua, jambo linalosababisha baadhi ya wachungaji kushindwa kuidhibiti mifugo hiyo na kuingia katika mashamba mengine.

Moja ya Shimo kubwa kati ya sita  yanadaiwa kutumika kama boma la ng'ombe na wafugaji jamii ya wamasai kuandaa mazingira kabla ya kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima kitongoji cha Sanya Line A Kata ya Mabogini Wilayani Moshi. Picha na Yese Tunuka

Kuhusu madai ya wananchi kushambuliwa, Mnzava amesema suala hilo sasa ni la jinai na linafanyiwa kazi na Jeshi la Polisi.

“Endapo kuna mtu ameshambuliwa au kujeruhiwa, hilo si suala la migogoro ya kilimo na mifugo pekee bali ni kosa la jinai ambalo linapaswa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua stahiki,” amesema.

Aidha, amesema tayari ameelekeza idara ya mifugo pamoja na Jeshi la Polisi kufuatilia kwa karibu hali ya eneo hilo na kuhakikisha sheria zinafuatwa.

Kuhusu madai ya rushwa yanayotolewa na baadhi ya wananchi, Mnzava amesema Serikali haiwezi kuthibitisha tuhuma hizo bila ushahidi, lakini imeahidi kufuatilia taarifa zozote zitakazowasilishwa ili kubaini ukweli wake.


Wafugaji

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Kanda ya Kaskazini, Lekei Ole Milakoni, amesema hajapokea malalamiko rasmi kuhusu tukio hilo, lakini amesisitiza kuwa mifugo kuingia katika mashamba yenye mazao ni kosa lisilokubalika.

“Ni kinyume cha sheria na hakiwezi kuvumiliwa. Mazao yanalimwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu na si chakula cha mifugo,” amesema.

Milakoni, amesema atafuatilia taarifa hizo kwa kushirikiana na viongozi wa wafugaji katika eneo husika ili kubaini ukweli wa malalamiko yaliyotolewa na wakulima na kusaidia kupatikana kwa suluhu ya kudumu.