Wakulima waonywa kuuza kahawa kimagendo

Muktasari:
Wakulima wa zao la kahawa mkoani Kagera wametakiwa kuacha tabia ya kuuza zao hilo kwa njia ya magendo kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwakuwa wana kiuka taratibu za nchi ikiwemo kuikosesha Serikali mapato.
Bukoba. Wakulima wa zao la kahawa mkoani Kagera wametakiwa kuacha tabia ya kuuza zao hilo kwa njia ya magendo kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kwakuwa wana kiuka taratibu za nchi ikiwemo kuikosesha Serikali mapato.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 28, 2023 kwenye mkutano wa 33 wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU- 1990 Ltd) mjini Bukoba, Katibu Tawala mkoani humo, Toba Nguvila amesema baadhi ya wanunuzi wamefikia hatua yakuvusha kahawa inayolimwa katika mkoa huo nje ya nchi.
“Acheni biashara za magendo, mfano kule wilayani Kyerwa baadhi ya wanunuzi wanaendelea na biashara hiyo na kudiriki kuvusha kahawa nje ya nchi, vyombo vya ulinzi na usalama viko makini kuhakikisha hilo haliendelei. Serikali haiitaji kuwatesa na kutaifisha kahawa ya wakulima hivyo tufuate taratibu za nchi,”amesema Nguvila
Amesema baada ya Serikali kuanzisha mfumo mpya wa kuuza kahawa kwenye mnada, msimu wa 2021/22 kilo moja iliuzwa Sh1,400 huku msimu wa 2022/23 ikiuzwaa Sh2,000 hivyo kuongeza kipato kwa mkulima na kuongezeka mapato serikalini.
Nguvila amewataka Maofisa Ugani, Bodi ya kahawa pamoja na Mrajisi Msaidizi wa vyama vya Ushirika mkoani humo kuhakikisha mzani wa rula ambao ulikuwa unatumika zamani hautumiki badala yake utumike mzani wa kidigitali.
Katika hatua nyingine, amewashauri wakulima kufuata taratibu zote za uvunaji wa kahawa ikiwemo kuhakikisha wanavuna iliyoiva pamoja na kutoanianika kwenye udongo ili iwe na thamani kulingana na viwango vya kimataifa.
Akisoma taarifa makisio kwa msimu wa 2023/24, Muhasibu Mkuu wa KCU - 1990 Ltd, Thatianus Kamai amesema chama hicho kinatarajia kukusanya kilo 12 milioni za kahawa ya robusta na makisio ya kahawa safi arabika na robusta zitakusanywa kilo 2.5 milioni.
Amesema Msimu 2022/23 walikisia kukusanya kilo 16 milioni lakini zilikusanywa kilo 9 milioni huku kahawa safi ikikusanywa kilo 2.3 badala ya kilo 2.4 milioni waliokisia.
Aidha amesema, bei ya msimu huu kwa kahawa ya kawaida itategemea mnada huku bei ya kilo moja ya kahawa hai robusta itaanzia Sh5,300 na arabika Sh4,700.