Wakulima wawachongea mawakala wa mbolea
Muktasari:
- Wakulima mkoani Njombe wamechongea mawakala wa mbolea mkoani hapa, na hii ni baana kuwepo kwa madai kuwa katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023; waliuziwa mbolea iliyochanganywa na mchanga, hivyo kuwasababishia hasara.
Njombe. Wakulima mkoani hapa, wameitaka Serikali kuwadhibiti mawakala wote wa mbolea ambao watabainika siyo waaminifu.
Ombi hili linatokana na hali ya sintofahamu, baada ya msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 ambapo baadhi ya wakulima mkoani humo walidai kuuziwa mbolea iliyochanganywa na mchanga, jambo liliwasababishia kupata mavuno duni.
Wakulima hao wamewasilisha ombi lao leo Jumamosi Desemba 2, 2023; kwenye mkutano wa wadau wa kilimo Nyanda za Juu Kusini, ulioandaliwa na kampuni ya mbolea ya Intracom.
Baadhi ya wakulima hao akiwemo Frank Mwenda amewataka mawakala wa mbolea kwa ujumla, kuepuka kuuza mbolea iliyochakachuliwa.
"Kwa hiyo Serikali isimamie zaidi hawa watu, watakaobainika kuchakachua mbolea wapate adhabu kali ili kuwa mfano kwa wengine na hivyo kuzuia jambo hilo kuendelea," amesema Mwenda.
Mkuu wa Wilaya ya Makete, Juma Sweda akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema mkoa huo una mahitaji ya mbolea zaidi ya tani 112.
Amesema uwepo wa kampuni hiyo ya mbolea, unatoa fursa kwa wakulima wa mkoa huo, kuongeza tija na kipato kwenye shughuli zao za kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Intracom, Nazaire Nduwimana amesema kiwanda hicho kupitia mbolea ya FOMI kina mchango mkubwa katika mapinduzi ya kilimo nchini.
"Huwezi kuzungumza kilimo bila ya kutaja mbolea na inayohitajika ni ile iliyo sahihi na inayoweza kumkomboa mkulima, kuinua kipato chake na kukuza uchumi," amesema Nduwimana.