Wakunga, wauguzi 4,166 kufanya mitihani Desemba 29, 2023

Kaimu Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Happy Masenga (Kulia) akizungumza kuhusu mitihani ya usajili wa leseni itakayofanyika Desemba 29, 2023.

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, lengo la mtihani huo ni kupima umahiri wa watahiniwa ili kupata wauguzi na wakunga wenye sifa.

Dodoma. Wauguzi na wakunga 4,166 wanatarajia kufanya mitihani ya usajili wa leseni ifikapo Desemba 29, 2023 katika vituo saba nchini.

Huu utakuwa mtihani wa 21 tangu Baraza lilipoanza kusimamia lenyewe, ingawa tangu mwaka 1953 walikuwa wakisimamiwa na Wizara ya Afya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 27 jijini hapa, Kaimu Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, Happy Masenga amesema lengo la mtihani huo ni kupima umahiri wa watahiniwa ili kupata wauguzi na wakunga wenye sifa.

Masenga amesema Baraza halitawavumilia hata kidogo watakaofanya udanganyifu wa namna yoyote na kwamba watahiniwa wote wanatakiwa kufika kwenye vituo walivyojiandikisha kesho Desemba 28, 2023 ili wapewe maelekezo.

"Idadi ya wanaofanya mtihani mwaka huu ni ndogo ukilinganisha na Desemba mwaka jana (2022), ambao walikuwa 4,600, lakini kwa mwaka huu tuna watahiniwa 248 ambao walikosa sifa mwaka jana na tutaendelea kuwaacha wasio na sifa hadi watakapopata sifa stahiki," amesema Masenga.

Kwa mujibu wa Msajili huyo, hadi sasa wakunga wenye leseni nchini wapo 49,994 ambao wanaendelea kuwafuatilia kwenye maadili yao ambayo amesisitiza jicho litawatazama hadi hao wanaokwenda kufanya mtihani keshokutwa.

Akijibu kuhusu matokeo kutoka haraka ili wauguzi na wakunga wawahi kuomba nafasi zaidi ya 50O zilizotangazwa na nchi ya Saudi Arabia, amesema wanafanya kazi kwa kuzingatia misingi yao, hivyo watahiniwa watapewa matokeo kama inavyopaswa.

Kwa wanaoshindwa mitihani wanaruhusiwa kurudia mara nyingi kadri wawezavyo hadi watakapofaulu mitihani hiyo ndipo watapewa leseni ingawa hupewa vibali maalumu vya kufanya mazoezi kwenye hospitali kubwa ili wajifunze.