Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walalamikia mwitikio hafifu wa washiriki maonyesho ya biashara Tanga

Mmoja wa wajasiriamali waliojitokeza kwenye maonesho ya 13 ya kibiashara katika viwanja vya Mwahako jijini Tanga akionesha moja ya bidhaa yake ya kibunifu. Picha na Mbonea Herman.

Muktasari:

  • Baadhi ya washiriki wameeleza wasiwasi wao kuhusu uwezo wa kurejesha gharama walizotumia kushiriki maonyeshoni ya biashara

Tanga. Idadi ya washiriki katika maonyesho ya 13 ya kimataifa ya biashara yanayofanyika katika viwanja vya Mwahako jijini Tanga, imepungua kutoka washiriki 400 katika miaka iliyopita hadi 120 mwaka huu.

Hali hiyo inadaiwa kusababisha baadhi ya washiriki wa ndani na nje ya Mkoa wa Tanga kulalamikia kushindwa kufikia matarajio yao ya kibiashara.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi katika viwanja hivyo umebaini mabanda mengi yakiwa wazi, tofauti na ilivyokuwa katika maonyesho yaliyopita tangu yalipoanza kufanyika miaka 13 iliyopita.

Baadhi ya washiriki wameeleza wasiwasi wao kuhusu uwezo wa kurejesha gharama walizotumia kushiriki maonyesho hayo, huku wakiwataka waandaaji kuongeza ubunifu na vivutio ili kuvutia washiriki na wageni zaidi katika miaka ijayo.

Baadhi ya taasisivzilizojitokeza kwenye maonesho ya 13 ya kibiashara jijini Tanga zikiwa zinasubiri kuwahudumia wananchi wanaojitokeza kwenye maonesho hayo. Picha na Mbonea Herman.

Mjasiriamali wa dawa za asili kutoka Mkoa wa Arusha, Rose Mvungi akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Juni 7, 2026 amesema maonyesho ya mwaka huu yamekuwa tofauti kutokana na kupungua kwa idadi ya watu wanaotembelea viwanja hivyo kutafuta fursa mbalimbali za biashara.

“Wenyeji wa hapa wanasema hakuna watu wa kutosha wanaofika, na pia barabara ya kufika hapa ni mbovu. Hali hiyo imeathiri mwitikio wa wananchi na kufanya biashara kuwa ngumu. Ikiendelea hivi, inaweza kuwakatisha tamaa washiriki wengi kushiriki katika siku zijazo,” amesema Mvungi.

Amesema waandaaji wanapaswa kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na kurejesha vivutio vilivyokuwapo awali, ikiwamo maonesho ya wanyama.

“Mwaka jana kulikuwa na wanyama na mwitikio ulikuwa mkubwa, lakini mwaka huu hakuna vivutio vya kutosha. Gharama niliyotumia kutoka Arusha kuja hapa si rahisi kuzipata tena kwa hali ilivyo,” amesema.

Kwa upande wake, Khadija Hassan mjasiriamali wa vipodozi anayeshiriki kwa mara ya kwanza, amesema kwa mujibu wa maelezo ya wenyeji aliowakuta, hali ya mwaka huu ni tofauti na ilivyokuwa katika miaka iliyopita.

Amesema licha ya kufanya biashara, kiwango cha mauzo hakijafikia matarajio yake kutokana na mwitikio mdogo wa wananchi.

“Ili maonyesho haya yawe na mvuto zaidi, matangazo yanapaswa kufanyika mapema na kwa upana. Eneo hili liko mbali na katikati ya jiji, hivyo watu wengi hawafahamu kinachoendelea,” amesema Hassan.

Flora Unjiro kutoka DD Ruhinda Limited, kampuni inayozalisha bidhaa za mkonge amesema matarajio yao mwaka huu hayajatimia kutokana na uchache wa wageni waliotembelea mabanda yao.

Ametaja changamoto kuu ni ubovu wa barabara, ukosefu wa matangazo ya kutosha na muda mfupi wa maandalizi.

“Tunatarajia mwaka 2027 barabara itakuwa imeboreshwa na matangazo kufanyika kwa kiwango kikubwa zaidi. Lengo la maonyesho haya ni kuunganisha kampuni na kuwaonyesha wananchi bidhaa mbalimbali,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa Maonesho ya Kibiashara ya Mwahako jijini Tanga wakiendelea kutoa huduma licha ya mwitikio mdogo wa jamii kutembelea maonesho hayo. Picha na Mbonea Herman.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo, Leopold Abeid amesema kupungua kwa mwitikio kunahusishwa na kukosekana kwa baadhi ya vivutio muhimu.

Amesema changamoto nyingine ni upungufu wa wafadhili mwaka huu pamoja na ujio wa Mwenge wa Uhuru mkoani Tanga, hali iliyosababisha baadhi ya halmashauri kushindwa kushiriki kikamilifu.

Amebainisha kuwa gharama za kusafirisha wanyama zimeongezeka kutoka Sh800,000 hadi Sh1.5 milioni kwa gari, huku ucheleweshaji wa vibali na michakato ya kifedha kutoka kwa wadau ukiendelea kuwa changamoto.

Amesisitiza umuhimu wa kuanza maandalizi mapema na kuhakikisha wadau pamoja na wafadhili wanatoa ushirikiano kwa wakati ili kuwezesha maandalizi kufanyika kwa ufanisi kabla ya maonesho kuanza.