Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Walichobaini madaktari wa Tanzania walioweka kambi tiba Comoro

Muktasari:

  • Timu ya madaktari bingwa kutoka Tanzania wametoa huduma za uchunguzi na matibabu katika matatizo ya mifupa, figo na kibofu cha mkojo, saratani za aina zote, moyo, mishipa ya fahamu, uti wa mgongo na mengineyo ambapo takriban wagonjwa 2,770 walihudumiwa.

Dar es Salaam. Madaktari wa Tanzania wamehitimisha kambi tiba nchini Comoro kwa kutoa huduma kwa wagonjwa 2,770 na kufanya upasuaji kwa wagonjwa saba, ikiwemo kuainisha fursa za ushirikiano katika sekta ya afya.

Katika kambi hiyo ya matibabu, wameweza kuwabaini wagonjwa 269 ambao wanahitaji rufaa za matibabu zaidi nje ya nchi hiyo.

Akizungumza katika hafla ya kuagana baada ya kuhitimisha kambi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) aliyekuwa Mkuu wa msafara huo, Dk Peter Kisenge amesema kambi hiyo imekuwa na ufanisi mkubwa.

Pia amesema mwitikio kutoka kwa wananchi wa Comoro umekuwa mkubwa ambapo waliojitokeza walikuwa ni wengi kuliko walioweza kupata huduma, licha ya madaktari hao kulazimika kufanya kazi hadi usiku nyakati zingine.

”Tumebaini uhitaji mkubwa wa huduma zetu, wapo ambao tumeona wanalazimika kupata rufaa kwa uangalizi zaidi. Tumekubaliana na wenzetu wa Hospitali ya El Maarouf kuwa kambitiba hii iwemo katika kalenda zetu za vipaumbele na pia tujenge mfumo bora wa kisasa wa rufaa za matibabu kwa wanaokuja Tanzania.

“Ili wakija nchini kwetu kusiwe na kadhia wanazopata na wawe wanajua kabisa utaratibu wa kufuata, pia tumebaini maeneo muhimu ya kushirikiana zaidi hususani katika kuleta wataalamu wa fani mbali mbali washirikiane na wenzao,” amesema Dk Kisenge na kuongeza kuwa JKCI iliratibu kambi hiyo.

Dk Kisenge pia ameeleza mazungumzo waliyofanya na Waziri wa Afya nchini humo Dk Nassuha Ousseni Salim kuwa yametoa mwelekeo mzuri wa azma ya Serikali ya Comoro kushirikiana na Tanzania kwenye maeneo kadhaa ikiwemo utoaji wa matibabu toka masafa ya mbali (Telemedicine) ambalo baadhi ya Taasisi za Tanzania wanaweza kutoa.

Kambi hiyo iliyoratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Comoro ilishirikisha Taasisi za JKCI, Taasisi ya Mifupa na Ubongo ya Muhimbili (MOI), Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Saratani ya Ocean Road na Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Katika hafla ya kuwaaga madaktari hao Waziri wa Ulinzi wa Comoro, Youssoufa Mohamed Ali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Tawala - CRC na Katibu wa Rais wa nchi hiyo ndiye alikuwa mgeni rasmi na kuhudhuriwa pia na Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Shirika la Afya Duniani na Mabalozi wa Libya na Saudi Arabia.

Pamoja na magonjwa mengine kambi hiyo ilitibu na kuchunguza matatizo ya saratani za aina zote, mifupa, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, figo na mifumo ya mkojo na matatizo ya uzazi, magonjwa ya wanawake na matatizo ya meno.