Walichokisema Rais Samia, Mufti Zubeir kuhusu Idd El Fitri

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zuberi muda mfupi kabla ya kuanza kwa ibada ya Eid El Fitri katika Msikiti Mkuu wa Bakwata (Mfalme Mohammed VI wa Morocco), Kinondoni Dar es Salaaam. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Mufti wa Tanzania ahimiza matendo mema kwa Waislamu nchini baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Dar es Salaam. Mufti wa Tanzania, Sheikh Mkuu, Abubakar Zubeir amesema sikukuu ya Idd El Fitri ni siku ya kutenda mambo mema na kushirikiana zaidi na sio siku ya kufungua milango ya kutenda maasi.

Sheikh Zubeir ameeleza hayo leo Jumatano Aprili 10, 2024 baada ya swala ya Idd El Fitri iliyoswaliwa kitaifa katika msikiti wa Mohamed VI, uliopo Kinondoni, Dar es Salaam iliyohudhuriwa pia na Rais Samia Suluhu Hassan, mawaziri na mabalozi.

"Siku ya Idd el- Fitri ni siku ya furaha, kuitana kushirikiana na kumuomba Mungu msamaha zaidi, sio siku ya kumuasi Mungu.

"Tumuombe Mungu turudi salama nyumbani, atusitiri na dhambi na aibu zetu na atukamilishie swaumu tulizofunga na malipo ya siku yetu ya Idd," amesema Sheikh Zubeir.

Katika hatua nyingine, Sheikh Zubeir amewaomba Waislamu kujitokeza kwa wingi kuhudhuria Baraza la Eid litakalofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, litakalohudhuriwa na Rais Samia kuanzia saa 10 alasiri.

Suala hilo pia lilitiliwa mkazo na mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Hassan Chizenga aliyesema siku ya Idd, Mungu anahimiza kutenda mambo mema, sio kurudi katika maasi.

Sheikh Chizenga amesema wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani mambo yalitulia, hivyo ni vema waumini wa dini hiyo kuendeleza matendo ya mwezi ya mwezi huo.

Mmoja wa waumini wa dini hiyo, Hassan Juma ameungana na viongozi hao kusisitiza Waislamu kutenda na kuendeleza mema baada ya mwezi wa Ramadhani, akisema kuna maana kubwa kwa Mungu kufanya hivyo.

Katika hatua nyingine, Rais Samia ametumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwatakia heri Waislamu na Watanzania kwa ujumla akisema: “Nawatakia Watanzania wote heri ya Sikukuu ya Idd el-Fitr, tukimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa baraka ya kuhitimisha funga na ibada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.”

“Mwenyezi Mungu atuonaye tunaposimama na mageuko yetu kati ya wanaosujudu, mwenye kusikia na kupokea dua zetu; aendelee kutubariki na kudumisha Taifa letu katika haki, umoja, amani na mshikamano; katika misingi ya kufanya yaliyo mema, kujali na kutumikia wengine kwa upendo na weledi na mioyo iliyojaa shukrani na ibada kwake. Idd Mubarak,” ameandika mkuu huyo wa nchi.

Katika Msikiti wa Mtoro –Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Sheikh wa msikiti huo, Abdallah Mohammed amewataka waumini kutumia mafundisho waliyopata katika kipindi cha chote cha mwezi mtukufu wa Ramadhani kudumisha amani katika uchaguzi wa kuwapata viongozi wa kitaifa.

Amesema chaguzi zinaambatana na mambo mengi ndani yake, lakini ili kuvuka salama na kumpata kiongozi sahihi, ni lazima kuwepo na tunu ya amani.

Shekh Abdallah amesema mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kama chuo, hivyo ni muhimu kwa waumini kuyaishi matendo mazuri waliyokuwa wanayafanya katika nyakati zote, ikiwemo uchaguzi ili kudumisha amani ambayo msingi wake ni ibada.

"Tunakwenda katika uchaguzi (uchaguzi wa Serikali za mitaa) kunakuwa na matatizo mengi ndani yake, ili tuvuke salama msingi wake ni amani kwa hiyo Waislamu wawe watulivu kama walivyokuwa kwenye mwezi mtukufu wa Ramadhani," amesema.

Shekh Abdallah amesema mafundisho wanayopata ndani ya mfungo yanawataka binadamu kutomuasi Mola wao, watu wakiwa na hisia hiyo hawawezi kuua, kuiba au kuwa mkorofi kwa kuamini akitenda Mungu atamuona.

"Tumewausia waumini na Watanzania wote tutumie mafundisho tuliyoyapata katika mwezi mtukufu wa Ramadhani, kwani Ramadhani ni kama chuo tuliyojifundisha na yale tunayojifundishwa tunapaswa kwenda kuyatumia ndani ya miezi 11 watu wawe na amani wasiwe wakorofi," amesema.

Kuhusu sikukuu hiyo, sheikh huyo amesema watu wanatakiwa kuwa na ushirikiano mzuri,  wafurahi na familia zao na watembeleane na kupeana zawadi.

Kwa upande wake, kiongozi wa msikiti huo upande wa vijana, Hamis Dotto amesema ibada hiyo ilikuwa nzuri kutokana na hotuba iliyotolewa na Shekh wao, Abdallah ya kuwataka kuishi kwa kuzingatia misingi ya funga na ibada zaidi.

"Yale yote tuliyoyaishi kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, tuyaishi muda wote kwa kuwa ni maagizo ya Mwenyezi Mungu hasa vijana tumekuwa tukinyoshewa vidole kufanya mambo yasiyofaa. Ni muhimu tuzingatie hotuba iliyotolewa kama somo," amesema.

Hamis amesema kumejengeka utamaduni wa watu ukiisha mwezi mtukufu wanaacha misingi na kuanza kufanya mambo yanayochafua taswira ya uislamu.