Walichokisema viongozi wa Chadema kuhusu siasa nchini Tanzania

Muktasari:

  • Unaweza kusema mazishi ya Meja Jenerali, Alfred Mbowe jana Ijumaa Agosti 2, 2019 yalichukua mrengo wa kisiasa, Chadema ikitumia fursa hiyo kutaka viongozi wawe makini na kudumisha amani.

Hai. Mazishi ya Meja Jenerali, Alfred Mbowe jana Ijumaa Agosti 2, 2019 yalichukua mrengo wa kisiasa, Chadema ikitumia fursa hiyo kutaka viongozi wawe makini na kudumisha amani.

Haikuishia hapo, Joseph Selasini ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini aliwaambia waombolezaji kuwa mwenyekiti wao,  Freeman Mbowe anahitaji maombi kwa kuwa anapitia kipindi kigumu.

Meja Jenerali Mbowe, ambaye ni kaka wa mwenyekiti huyo wa Chadema, alifariki dunia Julai 28, 2019 jijini Dar es Salaam na alizikwa jana katika Kijiji cha Nshara, Machame mkoani Kilimanjaro.

Akitoa salamu baada ya ibada ya mazishi iliyofanyika Usharika wa Nshara wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Selasini alisema Mbowe anapitia kipindi kigumu katika kuimarisha demokrasia nchini.

Mbunge huyo wa Rombo alisema katika kipindi hiki, Mbowe, ambaye pia ni mbunge wa Hai na kiongozi wa kambi ya upinzani Bungeni, anapaswa kuwa na busara na hekima kama ya Mfalme Suleiman.

“Tunamuomba Mungu amuimarishe Freeman Mbowe katika utumishi na kumpa busara kama alizompa Nabii Suleiman ili aweze kuendelea kuwa kiongozi mzuri katika familia na katika kipindi hiki kigumu ambacho anapitia kama kiongozi wa chama kitaifa,” alisema Selasini.

“Awe kiongozi mzuri katika harakati za kuleta maendeleo ya Jimbo la Hai, bila kujali tabia ambayo inaendelea ya kujijenga kwa baadhi ya viongozi, kuwanyanyasa, kuwatisha na kuwaweka mahabusu baadhi ya wadau wa maendeleo katika jimbo hili la Hai.”

Mbowe (57), amekuwa mbunge wa Hai tangu mwaka 2000 na mwenyekiti wa Chadema tangu 2004, akikiongoza kuwa chama kikuu cha upinzani na hata kupata asilimia 39 ya kura za urais katika uchaguzi mkuu mwaka 2015.

Hata hivyo, katika miaka ya karibuni amekuwa katika mizozo na mamlaka kuhusu biashara zake na pia kufunguliwa kesi ambazo chama hicho kinazitafsiri kuwa ni za kisiasa.

 

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumamosi Agosti 3, 2019