Walimu 285 watuhumiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi

Walimu 285 watuhumiwa kujihusisha kimapenzi na wanafunzi

Muktasari:

  • Serikali imesema walimu 285 kati 10,115 walifikishwa katika Tume ya Utumishi wa Ualimu (TSC) kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi na wanafunzi katika kipindi cha miaka minne.

Dodoma. Serikali imesema walimu 285 kati 10,115 walifikishwa katika Tume ya Utumishi wa Ualimu (TSC) kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi na wanafunzi katika kipindi cha miaka minne.

Hayo yalisemwa leo Septemba 7, 2021 na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Ummy Mwalimu wakati akikabidhi pikipiki kwa makaimu makatibu wasaidizi wa tume hiyo jijini Dodoma.

Amesema kuwa makosa hayo ni sawa na asilimia 2 ya makosa yote yaliyofikishwa katika tume hiyo katika kipindi hicho.

“Kwangu mimi nimeangalia makosa ya walimu katika kipindi cha miaka minne iliyopita asilimia 68 ya makosa ya walimu ni utoro,” alisema.

Amesema walimu 285 walibainika kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi kati ya walimu 10,115 sawa na asilimia mbili.

“Kwangu mimi mwalimu yoyote ambaye atakutwa na tuhuma na kudhibitika kwamba anauhusiano wa kimapenzi hatuta mvumilia niseme kama waziri lakini kama mama,”amesema.

Amesisitiza pia tume hiyo kuzingatia haki wanaposikiliza na kuamua rufaa za walimu na sio kufanya hivyo kwa upendeleo kwasababu wanamfahamu mhusika.

Ameitaka kutomuonea aibu mwalimu yoyote ambaye atakuwa amekiuka kanuni za utumishi wa walimu.

Aidha, Ummy alisema malalamiko ya walimu bado yapo na hivyo kuwataka kuyashughulikia kwa haraka.

Kwa upande mwingine, Waziri Ummy amesema Alisema malalamiko mengi yalikuwa ni juu ya upandaji wa madaraja ambapo asilimia 96 wamepanda madaraja katika kipindi hiki.

Halikadhalika Ummy ameagiza tume hiyo kutohamisha walimu hasa katika maeneo ya vijijini bila kuwa na walimu mbadala wa kwenda.

“Marufuku kubadilisha walimu tuliowapeleka halmashauri za pembezoni bila kupeleka walimu wengine mbadala,”amesema.