Walimu wasotea mshahara miaka 11 shule ya Wazazi

Muktasari:

  • Aidha, walimu hao wamekuwa na madai matatu dhidi ya mwajiri wao ambayo ni barua ya ukomo wa kazi, malimbikizo ya mishahara pamoja na mafao ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambayo michango yao haijawasilishwa.

Simiyu. Watumishi 14 wakiwamo walimu wa shule ya Jumuiya ya Wazazi ya CCM), Bulima Sekondari iliyopo Wilaya ya Busega mkoani Simiyu, wamekuwa katika sintofahamu baada ya shule hiyo kubinafsishwa bila kupewa taarifa.

Aidha, walimu hao wamekuwa na madai matatu dhidi ya mwajiri wao ambayo ni barua ya ukomo wa kazi, malimbikizo ya mishahara pamoja na mafao ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambayo michango yao haijawasilishwa.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed, alisema anafahamu madai hayo na anafuatilia ili kuyafanyia kazi.

"Madai yao yamekuwa yakijadiliwa katika vikao vya jumuiya ya wazazi na sisi kama chama, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu hivyo ninaomba niendelee kufuatilia ili nije na taarifa sahihi kuhusu madai hayo," alisema Shemsa.

Malalamiko

Wakizungumza na Mwananchi shuleni hapo juzi, walisema wamekuwa wakidai malimbikizo ya mshahara tangu mwaka 2012 shule hiyo ilipoanza kusuasua kuwalipa na ilifikia wakati walilipwa mishahara mitatu kwa mwaka.

Mary Mshana ni mmoja wa watumishi wa shule hiyo aliyeajiriwa mwaka 2007 kama katibu mukhtasi, tangu kuanza kuyumba kwa shule hiyo walianza kutolipwa mshahara kwa wakati na hatimaye kutolipwa kabisa.

"Ilitokea ukilipwa Januari unaweza kulipwa tena Julai Kwa mwaka tulikuwa tunaweza kulipwa mara tatu, ilipofika 2022 uchumi wa shule ulizidi kuyumba na wanafunzi walikuwepo 70, mwaka 2023 hatukupokea kabisa wanafunzi hivyo shule ikawa imejifunga," alisema.

Alisema kwa kipindi chote hicho walikaa kwa kutegemea maagizo ya uongozi wa juu wa jumuiya ya wazazi wa CCM, lakini hawakupata taarifa yoyote ambapo walianza kuzizungukia ofisi zake ili kupata barua ya ukomo wa kazi lakini waliambiwa waendelee kusubiri.

"Siku zinavyoenda mambo yanakuwa mengi, tumekuwa omba omba na kisaiklojia imeniathiri sana. Sina makazi ya kudumu wala sina chochote tumebaki kusubiri hatima bila mafanikio ninatamani kurudi nyumbani lakini hapa bado ninahesabika kama mfanyakazi maana sina barua ya ukomo," alisema Mary Mshana.

Bulima Sekondari ilianzishwa mwaka 1982 ikibadilishwa kutoka kuwa chuo cha ufundi Mwanza na mwaka 2004 ilikuwa na watumishi 36, 2014 watumishi 21, mwaka 2022 ilibaki na watumishi 14 kati yao walimu wakiwa sita.

Aliyekuwa mlinzi wa shule hiyo ambaye hakutaka jina lake litajwe hadharani, alisema aliajiriwa pale mwaka 2010 na ilipofika 2022 aliomba kustaafu kwa sababu za kiafya ambapo pamoja ma yote aliamua kudai haki zake kama mtumishi.

"Nilipoomba kupumzika ili nikashughulikie afya yangu nilitamani stahiki zangu za mfuko wa mafao zinisaidie lakini nilipofuatilia katika ofisi za NSSF niliambiwa michango yangu ili kuwa haijawasilishwa na mchango uliokuwepo tangu niajiriwe ilikuwa Sh300,000,"alisema mlinzi huyo wa zamani.

Alisema baada ya kufuatilia katika ofisi za jumuiya ya wazazi wa chama cha mapinduzi wilaya na mkoa hatimaye walienda ngazi ya taifa ambapo waliambiwa kuwa malalamiko yao yanafahamika na yanafanyiwa kazi waendelee kusubiri.

"Walisema wanafahamu hata michango yetu katika mfuko wa hifadhi ya jamii haikuwasilishwa vizuri hivyo wanaenda kutengeneza utaratibu mzuri ili kutulipa stahiki zetu na walisema kuwa wanaenda kuuza baadhi ya shule na bodinya wadhamini taifa imelipitisha hilo," Aliongeza mlinzi huyo.

Februari 06, 2023 katibu wa elimu na malezi Taifa kutoka Jumuiya ya Wazazi CCM, Joseph Ludovic alifika shuleni hapo kuongea na watumishi kisha kuahidi kulifanyia kazi mapema ili wapate sitahiki zao.

Jackson Kang'oma ni mwalimu wa somo la fizikia katika shule hiyo alisema kuwa shule ilipunguza wanafuzi kutoka 12000 mwaka 2004 jambo ambalo lilisababishwa na kudorora kwa usimamizi na uongozi hivyo hadi mwaka 2022 shule ilibaki na wanafunzi 70.

"Tunaomba tupatiwe malimbikizo yetu ya mishahara, barua ya ukomo wa ajira na michango yetu ya NSSF ili maisha mengine yaendelee, uchumi ni mgumu hatuna kazi hatujui hatma yetu," alisema mwalimu Kang'oma.

Tereza Mihayo ni mtumishi wa shule hiyo tangu 2007 na alisema bado wanaendelea kuishi katika nyumba za watumishi zilizopo katika shule hiyo wakiendelea kusubiri kulipwa stahiki zao.

"Jumuiya ya wazazi CCM Taifa haitaki kukubali kitulipa wala kutusikiliza na shule hii tayari inamwekezaji na wamefanya taratibu zote bila kututaarifu na hatujui nini kinaendelea walisema wanasubiri mkaguzi wa ndani afanye uhakiki ili tulipwe," alisema Tereza.

Jeremia Sweya aliyestaafu kazi katika taasisi hiyo alisema tangu amestaafu mwaka 2022 hajapata sitahiki yoyote kama mtumishi hali iliyosababisha ashindwe kurudi nyumbani kwani ni muda mrefu mwajiri hakumlipa mshahara na hajapata mafao ya kustaafu kutokana na kuwa michango yake haikuwasilishwa katika mfuko wa hifadhi ya jamii.