Walioachishwa shule waeleza mazito waliyopitia

Ritha Mahuwa aliyepata ujauzito akiwa kidato Cha kwanza na kurudi shuleni, akizungumza na Mwananchi kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari wasichana Msalato, Dodoma

Muktasari:

  • Ikiwa leo ni maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike, wasichana walioacha shule kwasababu ya ujauzito wametoa rai kwa wengine walioko mitaani kurudi shuleni ili kutimiza ndoto zao.

Dodoma. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mtoto wa kike Duniani, waliocha shule kwa sababu ya ujauzito wameeleza mazito waliyopitia kabla na baada ya kurudi shuleni.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi leo Oktoba 11, 2023 wasichana hao wamesema kubeba ujauzito ukiwa mwanafunzi ni uchungu usioelezeka ambao wanatamani watoto wengine wasiupitie.

Tangu Serikali iamue kuwarudisha kwenye mfumo wa masomo watoto walioacha shule kwa sababu mbalimbali, wasichana 7995 wamerudi shuleni ikiwemo waliopata ujauzito.

Akizungumza na Mwananchi Ritha Mahuwa amesema alipata ujauzito akiwa kidato cha kwanza mwaka 2013 uliomsababishia kuishi kwa manyanyaso kwa wazazi wake na kumuathiri kisaikolojia.

Ritha amesema mwanaume aliyempa ujauzito alimkataa na kusababisha kuwa mama wa nyumbani akijihusisha zaidi na kilimo Wilayani Mbinga, Ruvuma.

Ritha ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) amesema hali hiyo ilimfanya kukata tamaa kwani familia na jamii yake ilikuwa ikimtenga hali anayoileza kuwa na tamaa ya kujiua.

“Unapoacha shule kwa sababu ya ujauzito wewe ndio unaonekana mzembe na utapokea lawama zote kuanzia nyumbani hadi kwenye jamii unaweza hata kujiuwa kwa masimango, ni changamoto kubwa sana ambayo natamani watoto wa kike wasipitie”alisema Ritha

Mwaka 2019 Ritha alisikia fursa kwa Shirika la Karibu Tanzania Organization (KTO) ya kuwaendeleza watoto walioacha masomo.

Alisema Januari 2019 alijiunga na programu ya ‘elimu haina mwisho’ ambayo alifanikiwa kupata fani ya ushonaji huku akiendelea na masomo yake.

Ritha amesema changamoto nyingi alizopitia alizitumia kama chachu ya kusoma kwa bidii alipopata nafasi kwa mara ya pili hali iliyomfanya kupata wastani wa daraja la kwanza mtihani wake wa kidato cha nne mwaka 2020.

“Baada ya kufaulu masomo yangu nilipata wastani mzuri wa kuendelea na masomo na hapo ndugu yangu mmoja alijitokeza kunisaidia kunisomesha kidato cha tano na sita kwa mwaka mmoja mbapo pia nilifaulu kwa daraja la kwanza na kwenda chuo kikuu,” amesema.

Ritha amesema kwasasa anatarajia kumaliza shahada yake ya ualimu ili kutimiza ndoto zake za kuwa mwalimu wa Kiswahili.

Naye Neema Chaopa (21) ambaye amerudi shule baada ya kupata ujauzito akiwa kidato cha tatu amesema alikumbana na changamoto hiyo kutokana na ugumu wa maisha wa familia.

Neema amesema malezi ya mtoto katika umri mdogo ukiwa kwenye familia duni ni adhabu iliyokuwa mara mbili kwake na familia yake.

Neema amesema kutokana na hali duni na utoto, alishindwa kumpa malezi mtoto wake malezi kamili kama mama.

Mwaka 2022 Neema akiwa na shauku ya kuendeleza maisha yake, alijiunga na Taasisi ya elimu ya watu wazima Dodoma na sasa anatarajia kufanya mtihani wake wa kidato cha nne ili atimize ndoto zake za kuwa mwandishi wa habari.