Waliokumbwa na mafuriko Lindi waanza kupokea msaada

Muktasari:
Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Lulida ametoa tani nne za vyandarua 500 na maturubai 200 kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko katika kijiji cha Nanjima A na Nangaru Nanjima B mkoani Lindi.
Lindi. Mbunge wa Viti Maalum (CUF), Riziki Lulida ametoa tani nne za vyandarua 500 na maturubai 200 kwa wananchi waliokumbwa na mafuriko katika kijiji cha Nanjima A na Nangaru Nanjima B mkoani Lindi.
Lulida amesema ametoa msaada huo kutokana na wananchi wa Mkoa huo kukumbwa na mafuriko na baadhi kukosa makazi baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji.
“Mimi ni mbunge wenu wa viti maalum nimetoa msaada wa chakula, maturubai na vyandarua kwa sasa lakini wakati bado ninaendelea kuwaunga mkono na nitahakikisha tunashirikiana kipindi hiki cha shida,” amesema mbunge huyo.
Amesema wananchi hao wanahitaji msaada kwa kuwa kwa sasa wanakosa vitu muhimu.
Baraza Maduhu, alimshukuru mbunge huyo kwa msaada huo kwa maelezo kuwa utawasaidia na wataweza kujipanga upya, kuomba wapatiwe maeneo mengine wajenge nyumba na kuondoka maeneo ya mabondeni.
Mkuu wa Wilaya Lindi, Shaibu Ndemanga amesema mbunge huyo ameonyesha kuwathamini wananchi wenye matatizo.
"Tunahitaji misaada wa chakula, nguo, dawa na hadi sasa tuna kambi nne za watu zaidi 843 waliokumbwa na mafuriko katika vijiji vya Mkoa wa Lindi,” amesema Ndemanga.
Amesema Serikali imetenga maeneo na wananchi wote waliokumbwa na mafuriko watapewa viwanja ili kuendeleza shughuli zao.