Waliosoma Old Moshi kukutana shule ikiadhimisha miaka 100 tangu ianzishwe

Baadhi ya majengo ya shule ya Sekondari Old Moshi iliyopo wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Muktasari:
- Shule ya Sekondari ya Old Moshi iliyopo wilaya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro itatimiza miaka 100 Oktoba 20, 2022 siku ambayo itawakutanisha viongozi wa kada mbalimbali wa serikali pamoja na wafanyabiashara waliosoma katika shule hiyo.
Moshi. Shule ya Sekondari ya Old Moshi iliyopo wilaya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro itatimiza miaka 100 Oktoba 20, 2022 siku ambayo itawakutanisha viongozi wa kada mbalimbali wa serikali pamoja na wafanyabiashara waliosoma katika shule hiyo.
Miongoni mwa wafanyabaishara maarufu waliosoma katika shule hiyo ni aliyekuwa mmiliki wa makampuni ya IPP Media, marehemu Reginald Mengi na mdogo wake, Benjamin Mengi.
Akizungumzia maadhimisho hayo mkuu wa shule hiyo, Samwel Bendera amesema watakutana waliosoma katika shule hiyo ili kufahamiana na kuweka mikakati ya kuchangia mfuko wa pamoja wa kuisaidia shule hiyo.
"Tunatarajia kuwa na kilele cha maadhimisho ya miaka 100 ya shule yetu ifikapo Oktoba 20 mwaka huu, lengo la msingi ni kuwakutanisha wote waliosoma hapa ili waweze kufahamiana na kuikumbuka shule yao, kuweka mkakati wa pamoja wa kuona ni jinsi gani ya kuchangia mfuko wa pamoja kusaidia maendeleo ya shule," amesema mwalimu Bendera.
Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho hayo, Leila Shangali amesema wataweka mikakati endelevu ya namna bora ya kuboresha shule na kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.