Waliowakataa watoto Serengeti wazungumza

Serengeti. Wazazi sita wilayani Serengeti waliokataa kupokea watoto wao waliokimbia ukeketaji wametoa sababu tofauti ikiwemo kudai kuwa fomu walizopewa kusaini kuwalinda watoto hao kuwa zinawabana.

Watoto 53 walipokelewa katika Kituo cha Hope for Girls and Women Tanzania wilaya ya Serengeti wakikimbia ukeketaji kuanzia Novemba hadi Desemba 2020 na Januari 2021 walirudishwa nyumbani ili waendelee na masomo yao.

Mmoja wa wazazi hao sita, Mwita Wambura alidai kuwa masharti ya kusaini fomu kuwa hatamkeketa kwake ni magumu kwa kuwa mtoto huyo anaweza kurubuniwa na kukeketwa kisha akakamatwa yeye.

“Hapa kijijini wamekeketwa watoto wengi katika msimu wa mwaka jana waliobaki ni wachache tena ni 12 waliokimbilia mjini nadhani ndiyo waliobaki sasa wanaweza kwenda kisimani wakawa wanawatania kuwa ni wachafu wakashawishika kukeketwa mimi nikakamatwa,” alisema na kuongeza kuwa atamkubali bila ya masharti kwa kuwa hakuwa na mpango wa kumkeketa.

Joshua Mwita alisisitiza kuwa mtoto wake wa darasa la saba lazima amkekete ili aweze kuolewa haraka”

‘‘ Nasema lazima nimkekete maana dada yake sikumkeketa akasoma na kumaliza kidato cha sita akaolewa na Mjaluo wa Kenya huko sikupata ng’ombe,” alisema na kuongeza kuwa kama angekeketwa angeolewa na Wakurya na kupata ng’ombe.