Wazazi wawakana watoto wao waliogoma kukeketwa

Wazazi wawakana watoto wao waliogoma kukeketwa

Muktasari:

  • Wazazi sita wilayani Serengeti wamegoma kuwapokea watoto wao waliokimbia ukeketaji mwezi uliopita kwa madai kuwa bila kufanyiwa kitendo hicho hawawezi kuolewa.

Serengeti. Wazazi sita wilayani Serengeti wamegoma kuwapokea watoto wao waliokimbia ukeketaji mwezi uliopita kwa madai kuwa bila kufanyiwa kitendo hicho hawawezi kuolewa.

Mbali na kugoma kuwapokea, wamekataa kusaini fomu zinazowataka wasiwafanyie watoto wao kitendo hicho.

Watoto hao sita ni kati ya 53 walipokelewa katika Kituo cha Hope for Girls and Women Tanzania wilayani hapa kati ya Novemba na Desemba mwaka jana baada ya kukimbilia polisi wakipinga kukeketwa na Januari mwaka huu walirudishwa majumbani mwao ili kuendelea na masomo lakini wazazi wao wamegoma kuwapokea.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu amesema atawaita wazazi wote waliokaidi kuwachukua watoto wao ili wakabidhiwe mbele yake kwa masharti magumu zaidi.

“Kwanza tumewatunza na wapo salama, walipaswa kuwapokea ili waendelee na masomo. Nitawaita hapa niwape msimamo wa Serikali kwa maana hatuwezi kuruhusu watu wafanye ukatili kwa kuitisha Serikali, hilo linafanyika hivi karibuni, “alisema.

Mwita Wambura mkazi wa Kijiji cha Sogoti alisema masharti ya kusaini fomu kuwa hatamkeketa bintiye kwake ni magumu kwa kuwa mtoto huyo anaweza kurubuniwa na kukeketwa kisha akakamatwa.

“Hapa kijijini wamekeketwa watoto wengi katika msimu wa mwaka jana waliobaki ni wachache tena ni 12 waliokimbilia mjini nadhani ndiyo waliobaki, sasa wanaweza kwenda kisimani wakawa wanawatania kuwa ni wachafu wakashawishika kukeketwa mimi nikakamatwa.”

“Nitampokea kama watakubali kunipa bila masharti maana mimi sikuwa na mpango wowote wa kumkeketa yeye akatoroka, nikafuatilia polisi hadi kwa DC. Mimi nakuambia mpaka sasa sitaki kufuatilia maisha wala maendeleo yake labda mwalimu wake maana siwezi kupewa mwanangu kwa masharti,” alisema.

Joshua Mwita mkazi wa Kijiji cha Itununu yeye alisisitiza kuwa mtoto wake wa darasa la saba lazima amkekete ili aolewe haraka.

“Nasema lazima nimkekete maana dada yake sikumkeketa akasoma na kumaliza kidato cha sita akaolewa Kenya, sikupata kabisa ng’ombe,” alisema.

Alisema kama angekuwa amemkeketa angeolewa na angepata ng’ombe, kusisitiza kuwa lazima amkekete na akisoma aishie kidato cha nne aolewe maana soko lao ni kubwa.

“Kwa kweli nasisitiza kuwa lazima akeketwe na kutimiza hitaji la mila kitendo cha dada yake kilinifedhehesha sana kuchukuliwa na mtu wa Kenya kwa madai kuwa yeye amempenda ni msomi mwenzake wakati mimi sikumpenda hakikunifurahisha,” alisema.

Masonoro Marwa, mwenyekiti wa wazee wa mila wa ukoo wa Inchugu Tanzania na Kenya alisema kwa mila na desturi uamuzi wa kukataa watoto si mzuri.

“Hao wanataka kuitisha Serikali ili isiwabane wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa polisi maana wana dhamira ya kuwakeketa,” alisema.

Baadhi ya watoto waliokataliwa walidai kuwa walikimbia kwa kuwa maandalizi ya ukeketaji yalikuwa yamekamilika. Baadhi walihifadhiwa Shirika la Hope.

“Natakiwa kukeketwa ili niolewe, kaka yangu ambaye anasoma Sekondari ya Nyamoko apate mahari ya kuolea ndiyo maana naye anaungana na wazazi kuhakikisha nakeketwa, Desemba waliandaa hadi nguo nikatoroka,” alisema wanafunzi mmoja.