Wamekubali

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba (kulia) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dodoma juzi. Wengine kuanzia kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Innocent Bashungwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri MKuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene. Na Mpigapicha Wetu

Muktasari:

  • Baada ya kimya cha takribani wiki mbili kuhusu mjadala wa tozo za mialama ya simu na benki, Serikali imekiri maoni yaliyotolewa kuhusu tozo hizo kuwa, ni ya msingi na itayafanyia kazi ndani ya kipindi kifupi.

Dodoma/Dar. Baada ya kimya cha takribani wiki mbili kuhusu mjadala wa tozo za mialama ya simu na benki, Serikali imekiri maoni yaliyotolewa kuhusu tozo hizo kuwa, ni ya msingi na itayafanyia kazi ndani ya kipindi kifupi.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema hayo juzi, alipofafanua hoja za malalamiko ya mzigo wa tozo kwa wananchi.

Kauli hiyo ya Dk Mwigulu imekuja baada ya Gazeti la Mwananchi kwa siku kadhaa kutoa habari za malalamiko ya wananchi, ushauri wa wataalamu wa uchumi kuhusu kutozwa tozo kwenye miamala yote ya kielektroniki.

Jana, mawaziri wanne wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), George Simbachawene, walijitokeza mbele ya waandishi habari jijini Dodoma kuzungumzia tozo hizo.

Katika mkutano huo wa Waziri Simbachawene aliyeuongoza, wengine waliokuwepo kujibu hoja kuhusiana na tozo ni Dk Mwigulu, Profesa Joyce Ndalichako (Kazi, Ajira, Vijana na wenye Ulemavu) na Innocent Bashungwa (Tamisemi).

Awali, Simbachawene kabla ya kumkaribisha Dk Mwigulu kuzungumza, alisema kuchelewa kwa Serikali kutoa majibu kulikuwa ni makusudi ili kupata maoni ya wananchi na wataalamu wa uchumi.

Alisema juzi walikutana na wadau, vikiwamo vyama vya wafanyakazi na wachumi kujadiliana namna ya kupata ufumbuzi wa malalamiko hayo.

Wataalamu wa uchumi wamezungumzia ufafanuzi huo wa Serikali na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi alisema kitendo cha Serikali kupokea maoni ya wadau kinaonyesha ni sikivu na imekuwa ikifanya hivyo mara kadhaa.

Hata hivyo, aliitaka Serikali kushirikisha wadau kabla ya kupitisha tozo ili kupunguza malalamiko wakati wa utekelezaji wake, lakini pia ipange viwango vya tozo ambavyo ni himilivu.

“Hilo ni fundisho kwenye masuala kama haya, wawe wanawahusisha wataalamu, kuwe na majadiliano kati ya wadau na Serikali, waseme tunataka kufanya hiki, mnaonaje?” alisisitiza Profesa Moshi.

Mtaalamu huyo wa uchumi alisema Serikali ipanue wigo wa kodi ili watu wengi zaidi waweze kulipa kodi kwa kadiri ya kipato anachokipata.

Pia, alisema viwango vidogo vya kodi vitapunguza ukwepaji wa kodi.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Abel Kinyondo alisema Bunge linapopitisha tozo, watu wanaelekeza akili zao kwenye mambo mengine kama kodi ya pombe au mawigi na kusahau masuala ya tozo.

“Ukweli ni kwamba bajeti ni moja kati ya sheria, yaani Bunge kazi yake ni kutunga sheria na moja kati ya kipande kinachoitwa sheria ni bajeti. Sasa Tanzania tuna tatizo la kutokuwa serious na ufuatiliaji na kuwa makini wakati bajeti inasomwa, inajadiliwa na kupitishwa,” alisema Dk Kinyondo.

“Ili mradi ilipitishwa kwenye Bunge, tafsiri yake ni mbili; moja, ikiwa imepitishwa kwenye Bunge maana yake imepitishwa na wawakilishi wetu, maana yake sisi indirectly (sio moja kwa moja) tumeipitisha kwa sababu hata walipopiga kura sisi hatukwenda kuilalamikia.

“Lakini jambo la pili, ikiwa imepitishwa kwenye Bunge, maana yake katika mahesabu ya Serikali, hiyo tozo lazima ikusanywe tu kwa sababu ni chanzo kimojawapo cha fedha kilichopitishwa. Kwa hiyo, kwa sasa hivi yeye (Waziri) asipoikusanya, anavunja sheria,” alisema Dk Kinyondo.

Mhadhiri wa Chuo cha Biashara, (CBE) Dk Nasibu Mramba alisema tozo hiyo inamaanisha Mtanzania ataendelea kuumia kwa kuwa mfanyabiashara akitozwa fedha hiyo atahamishia mzigo kwa mwananchi wa chini.

“Ina maana mfanyabiashara hatakubali akatwe tozo hiyo, akikatwa Sh20,000 hiyo anaihamishia kwa mwananchi na mwisho wa siku tozo hiyo anayeenda kulipa ni yule mwananchi wa mwisho kabisa,” alisema.

Alisema kwa sababu tozo zimekuwa nyingi na zinaumiza, Serikali inatakiwa kusimamia vyanzo vya mapato vilivyoko.

Dk Mramba alisema katika vyanzo ilivyonavyo, Serikali imekuwa ikikusanya kwa kati ya asilimia 40 hadi 60 na kwamba hakuna chanzo ambacho kimewahi kukusanywa kwa asilimia 100.

“Kwa mfano kwenye maduka bado watu hawatoi risiti za EFD (risiti za kielektroniki), baadhi ya private sector hazilipi peyee, kampuni bado zinafanya ujanja, kwa hiyo namba moja ilikuwa ni kuhakikisha vyanzo vilivyopo vinakusanywa kwa asilimia 90 au 100,” alisema Dk Mramba.

Alishauri jambo jingine ni kubuni vyanzo vipya kwa kuwekeza katika utafiti wa vyanzo vipya vya mapato kwa sababu bado vipo vyanzo vya kuweza kupata fedha.

Alisema Serikali inaonekana ina matumizi yasiyo ya lazima, ikiwamo ununuzi wa magari yenye gharama kubwa, ofisini kuna wafanyakazi ambao utendaji wao uko chini, magari kunguruma wakati wote, makongamano, matamasha na semina.

Alishauri Serikali kubana katika maeneo ya matumizi halafu ndipo wamtoze mwananchi kiasi kidogo cha fedha.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Lousilie alipongeza hatua ya Serikali kutoa ufafanuzi kuhusiana na malalamiko hayo kwa sababu imeonyesha kuwa wanasikia vilio vya Watanzania.

Hata hivyo, alishauri Serikali kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuepuka vyanzo vinavyoleta malalamiko mengi kutoka kwa wananchi.

“Waziri akae chini na wataalamu wake kutambua vyanzo vipya vya mapato ambavyo vipo nchini. Watu wanasikia nchi yetu imejaa utajiri kila kona. Hii itasaidia Serikali kuondokana na vyanzo vinavyoleta malalamiko kwa wananchi mara kwa mara,” alisema Dk Lousilie.

Pia, alishauri uwepo wa matumizi yenye nidhamu kwa fedha zinazopatikana kutoka katika vyanzo vilivyopo kwa sababu watu wanaona baadhi ya watu wanavyofaidi kwa matumizi ambayo yangeepukika.

Dk Mwigulu na tozo

Akizungumzia tozo, Dk Mwigulu alisema Serikali imeanza kuyafanyia kazi mambo matatu yaliyolalamikiwa ambayo ni tozo kwenye miamala yote ya kielektroniki, taasisi za kifedha kuanza kukata tozo hiyo mapema kabla ya wakati na wapangaji kutakiwa kulipa kodi ya pango.

Alisema Serikali imesikia kilio na malalamiko ya wananchi wake kuhusu vipengele kadhaa vinavyohusiana na tozo.

Dk Mwigulu alisema, mfano wa hoja ni uwepo wa makato mara mbili kwenye miamala ya simu wakati wa kutuma na kutoa, hivyo muda si mrefu hatua stahiki zitachukuliwa.

Alisema kuhusu tozo za benki, Serikali itakaa na watoa huduma hiyo ili kujadiliana tena kwa mara nyingine.

Kuhusu kodi ya pango, alibainisha mpangaji siyo mdaiwa, bali yule mwenye nyumba, hivyo haitawahusu wao.

“Ili kuondoa mgogoro kati ya wapangaji na mwenye nyumba, Serikali itazingatia maoni ya watu waliopendekeza kuwaondoa wapangaji kwenye kadhia hii ili Serikali idai moja kwa moja kwa wamiliki wa nyumba,” alisema Dk Mwigulu.

“Lengo la kodi hii (ya pango) ni zuri, lakini kulikuwa na upungufu kwenye mkakati wa ukusanyaji wake, hivyo wao kama Serikali watajitathimini kuona wanafanyaje,” alisema Dk Mwigulu.

“Tumepokea maoni na tumekutana na makundi mbalimbali, shirikisho la vyama vya wafanyakazi wamekuja na maoni mazuri kabisa, tumekutana na wataalamu binafsi wa masuala ya kodi tumepata maoni yao, tumefuatilia takwimu na taarifa mbalimbali,” alisema.


Tucta yazungumza

Gazeti hili lilizungumza na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) kuhusu ufafanuzi huo wa Waziri Mwigulu na kusema tozo ya miamala ya benki ni sawa na kumtoza mfanyakazi kodi mara mbili.

Katibu Mkuu wa Tucta, Henry Mkunda alisema walipeleka malalamiko ya wafanyakazi kuwa tozo zinazotozwa kwenye miamala ya benki si rafiki kwao.

“Mishahara waliyolipwa wafanyakazi inakuwa imeshakatwa payee (kodi ya mishahara) lakini take home (kiasi kinachobakia) ambacho hupelekwa benki tena kinakatwa kodi. Kutokana na maoni tuliona sio sahihi sana kwa sisi wafanyakazi na kuamua kwenda kupeleka malalamiko yetu,” alisema Mkunda.

Alisema baada ya hapo Waziri Mwigulu alikubaliana nao kuwa hoja zao zina mantiki na mashiko na kuahidi kuyachakata kuona nini kifanyike.

Hata hivyo, alisema Dk Mwigulu alishauri kutafutwa ufumbuzi wa muda mfupi na mrefu; na kwa ufumbuzi wa muda mfupi walisema Serikali itakwenda kulifanyia kazi.

Katika ufumbuzi wa muda mrefu ni kuona wafanyakazi wanashiriki kwenye mchakato mzima wa maandalizi ya bajeti.


Chimbuko la tozo

Dk Mwigulu alisema chimbuko la tozo ni kwa ajili ya kuunganisha nguvu ili kutekeleza mahitaji ya lazima ambayo hayamo kwenye bajeti ya Serikali.

Alitoa mfano wa mahitaji hayo kama ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, vituo vya afya na kwamba uhitaji wa bajeti ni mkubwa, mfano ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere unaogharimu Sh6 trilioni, ujenzi wa reli ya kisasa unaogharimu Sh23 trilioni na kukaribia Sh30 trilioni.

Dk Mwigulu alisema mambo mengi yamefanyika na yanahitaji fedha, hivyo wakaona wapunguze kiwango cha tozo iliyoanza kwa Sh10,000 hadi Sh7,000 na baadaye Sh4,000, lakini kwa kuongeza wigo wa uchangiaji na ndipo benki zilipoingizwa.

Alisema wanatambua machungu yanayotokana na tozo, lakini lazima Watanzania wabebe jukumu la msingi la kuleta maendeleo ya Taifa, hasa kupitia miradi ya kimkakati ya maendeleo inayotekelezwa.

“Ni tozo, ndiyo, ina maumivu ya hapa na pale, ndiyo na tunatambua kweli kwamba inavuruga ‘purchasing power’ (uwezo wa manunuzi) ya mtu mmoja mmoja, lakini tuna majukumu ambayo kama nchi na sisi wote kama wazazi tunawajibika kuyabeba kama wajibu wetu,” alisema Dk Mwigulu.

Alibainisha mapato ya tozo katika mwaka wa fedha 2021/22, yalikuwa Sh221 bilioni zilizokwenda kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na Sh117 bilioni zilizojenga vituo vya afya.

“Tozo hii si kodi ya biashara wala si kodi inayotokana na faida ya biashara, bali chimbuko lake ni ushirikiano wa pamoja kuunganisha nguvu ili tuweze kupata rasilimali tutekeleze majukumu hayo ambayo ni ya lazima,” alisema Dk Mwigulu.

“Tozo hizo zimeendelea mwaka huu wa 2022/23 kwa sababu kuna majukumu ya msingi ambayo Serikali haiwezi kuyaahirisha.”

Hata hivyo, aliwataka wananchi kuendelea kushiriana na Serikali katika ujenzi wa miradi ya maendeleo.

“Mwaka huu tuliendelea tena (na tozo) kwa sababu tuna majukumu ya msingi ambayo hatuwezi kuyaahirisha. Hapa tulipo hatuwezi kuahirisha Bwawa la Nyerere, hatuwezi kuahirisha reli ya kisasa na matunda yake mtayaona baadaye,” alisema.

Dk Mwigulu alisema mwaka huu Serikali imepanga kujenga madarasa yasiyopungua 8,000 ili wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2023, wakae vizuri kwenye madarasa.


Tatizo la ajira

Dk Mwigulu alisema mwekelezo wa Serikali ni kuwekeza kwenye shughuli za uzalishaji kwa lengo la kutatua tatizo la ajira nchini.

Alisema mwaka huu wa fedha, Serikali imetoa Sh924 bilioni kwa ajili ya Wizara ya Kilimo na fedha nyingi zimeelekezwa kwenye kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kutengeneza ajira.

Dk Mwigulu alisema Serikali imeelekeza Sh100 bilioni kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi na Sh45 bilioni zimetolewa kwa ajili ya wamachinga na yote hiyo, imelenga kutatua tatizo la ajira.

Imeandikwa na Noor Shija, Sharon Sauwa (Dodoma) na Peter Elias (Dar es Salaam).