Wanachama wa Chadema wampokea Lissu Morogoro

Makamu Mwenyekiti wa chama cha Demokrasia na maendeleo Chadema Tundu Lisu akipunga mkono kusalimia  wananchi mara baada ya kuwasili katika mkutano wa wananchi unaofanyika katika viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha Ndege. Picha Hamida Shariff

Morogoro. Wanachama wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema ) Mkoa wa Morogoro leo Mei 7, 2023 wamejitokeza kumpokea Makamu Mwenyekiti wa hicho, Tundu Lissu ambaye amewasili mkoani humo na kufanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya shule ya msingi kiwanja cha Ndege.

Kabla ya kuwasili kwa Lissu baadhi ya viongozi wa chama hicho ngazi ya Mkoa walitoa salamu, akiwemo mwenezi wa Chadema Wilaya ya Morogoro, Shabani Dimoso amesema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha majimbo yote walioshindwa kwenye uchaguzi wa 2020 yanarudi.

Amesema moja ya mikakati ya chama hicho katika kuyarudisha majimbo hayo ni pamoja na kufanya mikutano katika kata zote.

Naye aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini, Devota Minja amesema kuwa miaka ya 1980 hadi 1990 Mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi vilivyokuwa vinazalisha ajira lakini kwa sasa vingi vimekufa na kusababisha wananchi kukosa ajira.

"Viwanda hivi vilijengwa na mbali ya kuzalisha ajira lakini pia vimekuwa vikiimarisha mahusiano kwa kuwa wananchi kutoka mikoa mbalimbali walikutana na kuoana na kutengeneza familia," amesema Devota.

Amesema kuwa kama viwanda vyote vilivyopo Morogoro vitafanyakazi vitasaidia kukuza uchumi wa mkoa mkoa wa Morogoro kwa kuwa vitaongeza fursa za kibiashara.