Lissu arejea nchini akiirarua Ripoti ya CAG

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu akizungumza katika moja ya mikutano ya chama hicho. Picha na Mtandao.

Muktasari:

  • Tundu Lissu arejea nchini na kutoa ahadi kwa wanachama wa Chadema kuwa amerudi kufanya kazi. Amegusia Ripoti ya CAG akieleza kwamba wizi na ufisadi ni uleule, mambo ni yaleyale hata ahadi ni zile zile.

Dar es Salaam. Waswahili wanasema ‘Mwenda kwao si mtumwa’ na ndivyo alivyofanya Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu baada ya kurejea nchini Tanzania leo Aprili 5, akitokea nchini Ubeligiji.

Makamu huyo ambaye ni mmoja kati ya watu muhimu katika Chama cha Demokorasia na Maendeleo (Chadema) baada ya kufika nchini ametoa salamu zake kwa wanachama wa chama chake huku akiwaahidi kuwa amekuja kufanya kazi, hivyo wajipange kwa mambo mazuri.

“Nimekuja nyumbani, hivyo wananchama wa Chadema wategemee kuwa Lissu amekuja kufanya kazi,” amesema.

Akizungumzia yale yaliyojiri kutokana na ripoti ya CAG, amesema “Wizi na ufisadi ni ule ule, kwa watu walewale, kwa chama kile kile, mambo ni yaleyale na ahadi ni zile zile,”

Awali, Lissu aliondoka nchini kwa mara ya kwanza Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 na watu wasiojulikana akitoka kuhudhuria vikao vya Bunge ambapo aliwahishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na kisha kupelekwa jijini Nairobi nchini Kenya.

Januari 6, 2018 alihamishiwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi hadi Julai 27, 2020 aliporejea nchini na kuwania urais lakini alishindwa na mgombea wa CCM, Hayati John Magufuli.

Hata hivyo Novemba 10, 2020, baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, Lissu aliondoka nchini kwenda Ubelgiji kwa madai ya kutishiwa usalama wake.

Lissu alirudi nchini Januari 25, mwaka huu akitokea Ubelgiji alikokwenda tangu Novemba 2020 akihofia usalama wake, ikiwa ni mwezi mmoja tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu.

Hata hivyo, Februari 15, mwanasiasa huyo aliondoka tena kwenda Ubelgiji na kuibua mijadala sehemu mbalimbali wakihoji sababu za kuondoka kwake.

Alipozungumza na Mwananchi, Lissu alisema alilazimika kurudi Ubelgiji kukutana na daktari wake na kurejesha visa yake iliyokwisha muda wake.