Wanafunzi Bunda walia ubovu wa barabara

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mariwanda wakipita kwenye barabara iliyojaa matope wakielekea shuleni. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

  •  Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mariwanda wamedai kuwa ubovu wa miundombinu ni kikwazo  kwo kufika shuleni kwa wakati

Bunda. Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mariwanda wameiomba Serikali kuboresha barabara ya shule yao ili iweze kupitika muda wote.

Pia, wameiomba kukarabati Daraja la Mto Mariwanda ambalo lina hatarisha maisha yao.

Wakizungumza na Mwananchi Digital Januari 10, 2024 wamedai kuwa ubovu wa miundombinu hiyo ni kikwazo  kwa  wanafunzi  kufika shuleni kwa wakati.

Mwanafunzi Agnes Mashindi amesema kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha barabara imejaa matope mengi hali inayowalazimu kuvua viatu ili waweze kupita.

"Tunavaa ndala au kupekua kabisa kwasababu hauwezi kupita kwenye hili tope ukiwa umevaa viatu, hii ni hatari kwa afya zetu kwa kuwa mbali na kupata magonjwa pia unaweza kujeruhiwa na kitu chenye ncha kali," amesema Mashindi.

Pia, amesema hali hiyo inawasababishia kuchelewa kufika shuleni.


"Zamani tulikuwa tunakwenda mbali sana kusoma kule Hunyari Sekondari, Serikali ikaamua kutujengea shule hapa karibu lakini sasa kuna changamoto kubwa ya barabara kujaa matope inatuchukua muda mrefu sana kupita kwenye tope hadi ufike shuleni,"  amesema mwanafunzi mwingine Anna Magembe

"Hali hii pia inasababisha tuonekane wachafu muda wote hata ukifua nguo  zako na kuzinyoosha ukitoka kwenye hilo tope unakuwa kama unatoka shambani," amesema.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda,  Salum Telela amekiri kuwepo kwa hali hiyo akisema Serikali inalifanyia kazi.

Amesema shule hiyo iliyojengwa kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari (Sequip) imegharimu Sh584 milioni na Serikali inalenga kuhakikisha inaboresha mazingira ya utoaji elimu kwa wanafunzi na walimu ili kuboresha taaluma.

"Barabara hii ipo kwenye bajeti ijayo lakini tayari nimemuagiza Meneja wa Tarura afanye ukarabati wa muda ili iweze kupitika wakati wakisubiri utekelezaji wa hiyo bajeti kwa sababu shule tayari imeanza na hatuwezi kukaa na hali hiyo hadi bajeti ijayo", amesema Telela.