Wanafunzi chuo cha uhasibu Arusha wahamia hoteli ya Ngurdoto

Wanafunzi chuo cha uhasibu Arusha wahamia hoteli ya Ngurdoto

Muktasari:

Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kuanzia leo Jumanne Desemba mosi, 2020 wataanza kutumia majengo ya hoteli ya kitalii ya Ngurdoto ambayo sasa yanatumika kama hosteli.

Arusha. Wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha kuanzia leo Jumanne Desemba mosi, 2020 wataanza kutumia majengo ya hoteli ya kitalii ya Ngurdoto ambayo sasa yanatumika kama hosteli.

Hoteli hiyo ilikuwa imefungwa kwa muda kutokana na kukosa wateja kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na watalii kupungua ikielezwa kuwa ni kutokana na ugonjwa wa corona kuyakumba mataifa mbalimbali duniani.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema hadi sasa  wanafunzi 1000 wamehamia katika vyumba vya hoteli hiyo yenye uwezo wa kulaza watu 2000.

"Mwanzoni tulipowatangazia kuhamia Ngurdoto wengi walikuwa wakisita lakini baada ya baadhi kufika sasa wengi wanaomba kuhamia na wamekuwa wakitumiana video za jinsi mandhari ya hoteli hiyo ilivyo,” amesema.



Amesema uongozi wa chuo ulilazimika kuanza kutafuta hosteli baada ya kupokea idadi kubwa ya wanafunzi mwaka 2020 na kwamba watakaolala katika hoteli hiyo watalipa Sh400,000 kwa mwaka na chuo kimeanza kutengeneza vitanda vya kutosha.

Baadhi ya wanafunzi wameeleza furaha yao kuhamia kwenye hoteli hiyo yenye bwawa la kuogelea na viwanja vya michezo mbalimbali.

"Hapa hakuna kisingizio ni kusoma mazingira ya bora wengine wanasema elimu na bata, "amesema Joseph Laizer mwanafunzi wa chuo hicho.