Wanafunzi vyuo vikuu, kati wahamasishwa kufanya utalii wa ndani

Mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Massana Mwishawa akizungumza katika kongamano la kuhamasisha utalii wa ndani kwa viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati mkoa wa Mwanza.

Muktasari:

  • Hifadhi za Taifa zinazopatikana katika Kanda ya Magharibi ni pamoja na Serengeti, Gombe, Kigosi, Milima ya Mahale, Burigi-Chato, Ibanda Kyerwa, Rumanyika Karagwe, Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane na Mto Gala.

Mwanza. Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) limewataka wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati nchini kufanya utalii wa ndani katika vivutio vilivyopo nchini ili kuchagia katika ongezeko la pato la taifa.

Wito huo umetolewa na mkuu wa hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa), Massana Mwishawa leo Januari 14 jijini Mwanza wakati akizungumza kwenye kongamano la kuhamasisha utalii wa ndani kwa viongozi wa serikali za wanafunzi katika vyuo vikuu na vya kati mkoani hapa.

Mwishawa amesema ushiriki wa wanazuoni katika utalii unahitajika ili kuongeza motisha kwa wananchi na kujijengea utaratibu wa kutembelea hifadhi za taifa.

Amesema mbali na hifadhi za taifa, wanazuoni pia wanamchango katika kuendeleza na kukuza uelewa wa mila na desturi za kitanzania ambazo ndiyo chachu ya kuvutia kuvutia watalii kutoka nje ya nchi.

“Tanapa imeanzisha kampeni ya kuhamasisha wanazuoni kushiriki katika utalii wa ndani kwa lengo la kuinua mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa kutoka asilimia 17 mwaka 2021 hadi asilimia kati ya 20 hadi 25 miaka mitano ijayo,” amesema Mwishawa

Ametaja hifadhi za taifa zinazopatikana katika Kanda ya Magharibi kuwa ni Serengeti, Gombe, Kigosi, Milima ya Mahale, Burigi-Chato, Ibanda Kyerwa, Rumanyika Karagwe, Kisiwa cha Rubondo, Kisiwa cha Saanane na Mto Gala.

Ameongeza: “Kampeni hii itakuwa ni endelevu ikiwa na lengo la kuhakikisha wanazuoni katika kila kanda wanakutanishwa na kujadiliana njia bora ya kuboresha mazingira yatakayoongeza motisha siyo tu kwao bali kwa Watanzania wote kuwa na utamaduni wa kutembelea hifadhi za taifa.”

Mkuu wa kitengo cha utalii hifadhi ya Saanane, Hilda Mikongoti amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wanafunzi zaidi ya 60,000 waliopo katika vyuo vikuu na vya kati mkoani hapa wanatembelea hifadhi za taifa angalau mara moja kwa mwaka.

“Mbali na wanafunzi hao, tuna wahadhiri (walimu wa vyuo) ambao pia kama wakijitokeza kutembelea vivutio vyetu tunaamini pato la taifa litaimarika,” amesema Mikongoji.

Naye Rais wa Chuo cha Utalii cha Taifa, tawi la Mwanza, Rosemary Range ametaja changamoto zinazokwamisha wanazuoni kufanya utalii wa ndani kuwa ni pamoja na uhaba wa magari, kukosa motisha, na kukosa bei elekezi ya gharama za kutembelea hifadhi husika.