Wanafunzi wa vyuo waaswa kuwa waadilifu
Muktasari:
Wanafunzi wa vyuo nchini wametakiwa kuwa waaminifu, waadilifu na wenye kujituma pindi wanapomaliza na kufanikiwa kupata ajira katika mashirika na kampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Dar es Salaam. Wanafunzi wa vyuo nchini wametakiwa kuwa waaminifu, waadilifu na wenye kujituma pindi wanapomaliza na kufanikiwa kupata ajira katika mashirika na kampuni mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Wito huo umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Mipango na Fedha wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) Dk Zainabu Mshani wakati akifungua halfa iliyowakutanisha wanafunzi na wadau mbalimbali kwa lengo la kujifunza na kuangalia soko la ajira linahitaji nini kwa sasa.
Amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa ili waweze kufanikiwa maishani ni muhimu kuwa waadilifu, wenye kujituma na waaminifu katika ufanyaji wa kazi ziwe za kuajiriwa au kujiajiri.
“Tunashukuru Mungu wanafunzi wetu wa NIT tumekuwa tukipata taarifa zao nzuri huko wanapofanya kazi kwamba ni watu wenye nidhamu, kujituma na waaminifu hii inatufanya tuweze kusonga mbele na kuendelea kuweka mikakati imara ya kukiimarisha chuo chetu.
“Sisi kama viongozi wa chuo tumekuwa tukifanya tafiti za kuangalia wanafunzi wetu wanauzika vipi sokoni na tumepata data za kutosha za kwamba wengi wapo kwenye kampuni mbalimbali na wanafanya vizuri,” amesema
Aidha amesema dunia ya sasa ni kubwa hivyo kama mwanafunzi hatakuwa na uwezo wa kuonyesha anaweza kiasi gani kufanyakazi hatoweza kupata fursa za kuajiliwa.
“Ndio maana tumeweka hafla hii hapa chuoni ambayo inakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya usafiri, mahinjinia na udhibiti viwango kwa lengo vijana kujifunza kutoka kwao lakini pia waoneshe bunifu zao na vile wanavyofundishwa chuoni. Kama nilivyosema dunia ni kubwa na ili uonekane unahitaji kuwa na uwezo wa kutosha,” amesema
Naye Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Jeremiah Kambei amesema katika hafla hiyo ambayo imeandaliwa na serikali yake, wanafunzi wanapata fursa ya kujifunza namna gani ya kujiandaa kukabiliana na changamoto ya ajira, kujiajiri pamoja na kujua mahitaji ya soko.