Wanafunzi waeleza adha ya usafiri mgomo wa daladala

Baadhi ya wanafunzi wakiwa wamesimama katika eneo la nje ya stendi ya Kilombero jijini Arusha wakisubiri usafiri kutokana na mgomo ulioanza jana wa daladala. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Mgomo huo wa tatu ndani yam waka huu, umeendelea katika baadhi ya maeneo licha ya uongozi wa madereva wa daladala kukutana Kamati ya Usalama ya Mkoa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa, John Mongela na kukubaliana kuusitisha.
Arusha. Baadhi ya wanafunzi wameeleza adha ya usafiri wanayopata kutokana na mgomo wa daladala ulioanza jana, wakisema wanachelewa na wengine kushindwa kabisa kufika shuleni.
Mgomo huo wa tatu ndani yam waka huu, umeendelea katika baadhi ya maeneo licha ya uongozi wa madereva wa daladala kukutana Kamati ya Usalama ya Mkoa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa, John Mongela na kukubaliana kuusitisha.
Wanafunzi jijini Arusha wameiomba serikali kuingilia kati mgomo wa daladala unaondelea katika jiji hilo kwani unawaathiri kwa sehemu kubwa katika masomo yao na kushindwa kufika shule kwa wakati.
Wakizungumza leo asubuhi Jumanne Agosti 15, 2023 baadhi ya wanafunzi hao wanaosoma shule ya Sekondari Suye iliyopo eneo la Moshono, wamesema gharama za nauli kwenda shule kwa kutumia usafiri mbadala wa pikipiki za magurudu matatu maarufu kama guta na bajaji zimepanda hadi kufikia Sh 1,000 hadi 1,500.
Awali nauli kwa wanafunzi kwa usafiri wa daladala ilikuwa ni Sh200 hivyo kuwa na ongezeko la kati ya Sh800 hadi Sh1, 300.
Mmoja wa wanafunzi hao, Ilham Hussein amesema kwa sasa wanapitia changamoto kutokana na kushindwa kulipa nauli kubwa huku guta nyingine zikiwashusha njiani.
"Tunapitia changamoto sana wakati wa kwenda shule, tunachelewa tunakosa masomo na wanatuonea sisi wanafunzi tunatozwa nauli hadi Sh1, 500 na wakati mwingine wanatushusha kwa njiani tunaomba mtusaidie suala hili ni gumu sana kwetu," amesema.
Naye Issa Abdallah ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha kwanza shule ya sekondari Suye, anasema changamoto ya usafiri imeaathiri kwani wengine wanalazimika kutembea kwa miguu hadi shuleni kutokana na kukosa daladala.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa jiji la Arusha wamesema Serikali ina haja ya kuingilia kati sakata hilo bila kumuonea mtu huruma na kama kuna anayehusika na suala hilo achukuliwe hatua.
Orest Mushi, amesema wanaomba serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, iangalie suala hilo ambalo kwa kiasi kikubwa kinaathiri wanafunzi.
"Wanafunzi hawa taifa la kesho, tutapata wapi Rais wa kesho kama Samia (Suluhu Hassan) au Julius Nyerere watatoka wapi? Madaktari tutawapata wapi, saa hizi ni muda wa saa tatu inakwenda wanafunzi bado ukiangalia hawajaenda," amesema.
"Tunaomba Serikali ichukue uamuzi mgumu kama kuna wanasiasa waliopo nyuma ya pazia juu ya jambo hili ijulikane, nyuma ya hili pazia la bajaji kuna nani, daladala imepangiwa na Latra nauli ya wanafunzi na abiria. Je, leo hii wanatozwa zaidi ya 1,000 hadi 1,500 itakuwaje?” amehoji.