Wanafunzi waliofutiwa matokeo wamuangukia Rais Samia
Mwanza. Wanafunzi 140 wa shule ya sekondari Thaqaafa ya jijini Mwanza waliofutiwa matokeo ya kidato cha nne wamemuomba Rais Samia Suluh Hassan kuwasaidia kurudia mtihani ili watimize ndoto zao.
Wanafunzi hao waliomaliza kidato cha nne mwaka jana ni miongoni mwa wanafunzi 337 waliofutiwa matokeo na Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kati ya watahiniwa wote 560,335 waliofanya mitihani ya kumaliza elimu hiyo.
Wanafunzi hao 140 ni kati ya 333 ambao walifutiwa na Necta kutokana na udanganyifu uliofanyika wakati wakifanya mitihani hiyo kati ya Novemba 14 hadi Desemba 1 mwaka jana.
Kati ya 333 waliofutiwa mmoja ni wa maarifa (QT) na 332 wa shule na kwa mujibu wa Necta wanafunzi hao wanayo fursa ya kurudia mitihani mwaka huu kama wanafunzi wa kujitegemea.
Mbali na rungu hilo kuwakuta wanafunzi hao, Necta lilivifungia vituo vitatu kuwa vituo vya mitihani ambavyo ni Andrew Faza Memorial cha Kinondoni Dar es Salaam, Cornelius cha Kinondoni na Mnemonic Academy cha Halmashauri ya Mjini Magharibi visiwani Zanzibar.
Februari 19, mwaka huu Waziri wa Elimu, Profesa Adolph Mkenda alikutana na wazazi na walezi wa watoto hao na kuwaahidi wizara hiyo itajadiliana kuangalia uwezekano wa kuwafanya warudie mitihani na kuwataka kuwa wavumilivu Serikali ikiendelea kutafuta mwarobaini wa sakata hilo.
Baadhi ya wanafunzi hao 140 waliozungumza na gazeti hili akiwemo Peter Andrew anayetamani kuwa daktari wa magonjwa ya binadamu alimuomba Rais Samia aangalie uwezekano wa wao kurudia mtihani kutokana na kutokujua hatima yao akidai kufutwa kwa matokeo kumewafanya wakate tamaa ya kutimiza malengo na ndoto zao za baadaye.
“Sisi tulifanya mtihani ipasavyo, tulifanya mtihani kwa uaminifu, tulijitahidi kusoma na wazazi wetu walituangaikia ili tusome, tufanye mitihani na matokeo yetu yatoke kwa ajili ya kuendelea kutimiza ndoto zetu.
“Wazazi wetu wengine ni wa hali ya chini ukizingatia shule yetu ilikuwa ni private, walitumia gharama kubwa kadri walivyoweza ili tusome na tumemaliza kwa amani lakini hatua ya mwisho tunaambiwa matokeo yetu yamefungwa kwa wizi wa mitihani. Tunamuomba mama Samia atusaidie,”alisema
Mwingine aliyefutiwa matokeo, Joba Sai alimuomba Rais Samia aingilie kati suala hilo akisema licha ya yeye kuumizwa na matokeo yake kufutwa na kujikuta akipoteza miaka minne bure shuleni pamoja na fedha za wazazi wake anaumia kuona wazazi wake wanavyoendelea kuhangaika ili atimize ndoto zake.
Naye Simon Tembe ambaye amemsomesha mtoto aliyekuwa akiishi mazingira ya mitaani lakini matokeo yamefutwa alimuomda Profesa Mkenda awape majibu kama alivyowaahidi kwenye kikao chake na wazazi hao huku akimuomba Rais Samia asaie watoto hao ili waendelee na masomo yao.
Mzazi mwingine, Thelathini Kimaro alisema wamepata taarifa watoto wengine wamekimbia majumbani mwao kutokana na jinsi ambavyo baadhi ya wazazi wamechukulia jambo hilo ikiwemo kuwalaumu akiomba Serikali itafute suluhisho kuokoa watoto hao.
Naye Upendo Alfred alisema wao kama wazazi wapo tayari kuchangia gharama ili watoto wao warudie mitihani huku mzazi mwingine, Ahida Abdallah akidai wameanza kuingiwa hofu watoto wao kujiingiza kwenye makundi yasiyofaa ikiwemo wizi, kuvuta bangi na ukahaba kwakuwa wapo mitaani bila shuguli yoyote na hawajui hatima yao kimasomo.