Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanafunzi walionusurika ajali ya Lucky Vincent wahitimu masomo yao

Vijana Wilson Tarimo, Sadia Awadh na Doreen Mshana wakati wa mahafari yao nchini Marekani.

Muktasari:

  • Ajali hiyo ilitokea wilayani Karatu wakati wakienda kufanya mitihani ya ujirani mwema, yakiwa ni maandalizi ya kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi. Ilisababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu na dereva.

Arusha. Wanafunzi watatu waliokuwa wakisoma katika Shule ya Msingi Lucky Vincent, wakanusurika katika ajali ya gari iliyotokea katika Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Mei 2017, wamehitimu masomo yao ya ngazi ya Stashahada ya Juu (Associate Degree) kwa muda wa miaka miwili nchini Marekani.

Waziri wa zamani, Lazaro Nyalandu alituma ujumbe kupitia mtandao wake wa kijamii wa Instagram, akiandika: “Wengi wetu tutawakumbuka watoto walionusurika ajali ya basi la Lucky Vincent, (Sadia, Doreen na Wilson) mwaka 2017. Sasa, kwa neema ya Mungu, wamehitimu Community College nchini USA na wataendelea na masomo ya juu katika vyuo vikuu.”

Mwananchi imezungmza na Nyalandu ambaye amethibitisha maelezo yake na kuongeza kuwa wamehitimu katika taasisi ya Western Iowa Technical Community College, Jimbo la Iowa nchini Marekani, na wataendelea na ngazi ya shahada ya kwanza kwa miaka miwili.

“Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa hatua waliyomaliza katika safari yao ya kufikia ndoto zao za elimu. Sasa wataendelea na ngazi ya shahada katika chuo hicho,” amesema Nyalandu.

Baada ya ajali iliyoacha simanzi, Sadia Awadh, Wilson Tarimo na Doreen Mshana walipata matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru. Baadaye ilionekana kuna haja ya kupata matibabu ya juu zaidi nchini Marekani, ambayo yaliokoa maisha yao.

Waliporejea nchini mwaka 2018, walijiunga na elimu ya sekondari katika Shule ya Star High School iliyopo wilayani Arumeru kupitia ufadhili wa Taasisi ya Siouxland Tanzania Education Medical Ministries (STEMM), kisha kurejea Marekani kwa masomo ya elimu ya juu.