Wanafunzi wanaorudia darasa na athari za kuacha shule

Wanafunzi wanaorudia darasa na athari za kuacha shule

Muktasari:

  • Idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi wanaorudia madarasa katika shule za serikali na zisizo za Serikali imeongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya miaka mitatu, Ripoti ya Elimu Msingi (Best) 2020 inaeleza.

Dar es Salaam. Idadi ya wanafunzi wa shule ya msingi wanaorudia madarasa katika shule za serikali na zisizo za Serikali imeongezeka zaidi ya mara mbili ndani ya miaka mitatu, Ripoti ya Elimu Msingi (Best) 2020 inaeleza.

Ripoti hiyo inayotolewa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (OR-Tamisemi) kila mwaka inaonyesha kuwepo kwa ongezeko la wanafunzi wanaorudia madarasa kwa sababu tofauti katika mwaka 2018 hadi mwaka 2020.

Kurudia darasa kumetajwa na wadau kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanafunzi kuacha shule kama ilivyomkuta Felix Bitambo.

Felix aliacha shule na kuingia katika shughuli ndogondogo baada ya kurudia darasa mara tatu mfululizo.

“Nikiwa darasa la tatu nilirudia, nikiwa la nne nilirudia, nilipoingia darasa la tano nikaambiwa nirudie nikaona siwezi kufanya kazi hiyo na nimeshajua kusoma na kuandika,” alisema Bitambo, akitaja sababu kubwa ni kuwa miongoni mwa waliofanya vibaya darasani.

Alisema kitendo cha kuacha shule kiliwakwaza wazazi wake, lakini baadaye walikuwa wakimuagiza afanye shughuli za shambani na kuangalia mifugo lakini hivi sasa ni dereva bodaboda anayetamani kurudi shuleni.

Ripoti inasemaje?

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanafunzi 379,683 walirudia darasa mwaka 2020 ikilinganishwa na wanafunzi 189,414 waliorudia mwaka 2018, ongezeko la karibia mara mbili.

Wadau wametaja wanafunzi hao kutokuwa na uwezo wa kuvuka madarasa waliyopo ni kutokana na uchache na uhaba wa vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

Mwaka 2020 wanafunzi wa darasa la tatu na nne ndio waliongoza kwa kurudia madarasa waliyokuwapo kwa idadi ya 94,687 na 117,762 mtawalia.

Hiyo ikiwa na maana kuwa wanafunzi wa darasa la nne pekee waliorudia walikuwa ni zaidi ya asilimia 31 ya wanafunzi wote waliorudia mwaka 2020.

Idadi hiyo pia ni ongezeko la zaidi ya asilimia 100 ikilinganishwa na wanafunzi 52,815 waliorudia darasa la nne mwaka 2018.

Ongezeko hilo halijaonekana tu kwa darasa hilo, bali pia katika madarasa mengine kumekuwa na ongezeko kwa viwango tofauti, huku darasa la saba ndiyo likiwa na idadi ndogo zaidi ya wanaorudia, likifuatiwa na darasa la tano.

Madarasa mengine yanayoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaokariri ni la kwanza, pili na darasa la sita.


Wadau wazungumza

Akizungumzia suala hilo, Catherine Sekwao, ambaye ni mdau wa elimu alisema kitu kinachoweza kupunguza tatizo hilo ni kuongeza idadi ya vifaa vya kujifunzia na kufundishia.

“Vitabu viongezwe mashuleni, zamani tulikuwa kitabu kimoja kwa wanafunzi watatu, sijui sasa hivi tumefikia wapi, hili linapaswa kuangaliwa ili wanafunzi wajifunze vizuri,” alisema Sekwao.

Alisema pia umakini na ufundishaji wa walimu na ubora wao unapaswa kuangaliwa ili kujua wanafundishaje.

“Zamani kulikuwa hakuna mwanafunzi aliyekuwa anatoka darasa la kwanza hajui kusoma, hii ni kwa sababu walimu waliokuwa wakifundisha madarasa haya walikuwa wanapewa mafunzo maalumu yanayozingatia K3, yaani kusoma, kuandika na kuhesabu.

“Siku hizi hili halipo, mwalimu yeyote anachukuliwa na kufundisha madarasa haya ya chini, yaani la kwanza na la pili,” alisema Sekwao.

Alisema pia utoro kwa walimu bado ni tatizo, kwani walimu wengi wamekuwa wakipumzika bila sababu za msingi, jambo ambalo linawafanya wanafunzi kushindwa kufundishwa kikamilifu na wanakosa baadhi ya vipindi.

Mtafiti wa Elimu, Muhanyi Nkoronko alisema wakati darasa la nne likiongoza kwa watoto wanaorudia, jambo hilo linaweza kuondolewa kwa kuboresha njia za ufundishaji.

“Kila mwanafunzi anaporudia darasa sisi watafiti huitafsiri kuwa ni kuongezeka kwa gharama, hivyo ni vyema mtoto afundishwe kikamilifu na anapotoka darasa moja kwenda jingine awe amepata maarifa, ujuzi stahiki utakaomwezesha kuendelea mbele,” alisema Nkoronko.

Alisema wakati mwingine mwanafunzi akirudia mara mbili darasa moja huacha shule kwa sababu anaona hafai kuendelea na darasa lingine.

“Kigezo kinachotumiwa kupima ni mitihani, tupunguze kutoka vigezo vya mitihani na tuje kwenye maarifa zaidi, ingawa kisera wamependekeza kuwa mtoto arudie mara moja akifeli ya pili apandishwe darasa,” alisema Nkoronko.

Alisema hii pia ni kati ya sababu zinazofanya wanafunzi waache shule, kwani kurudia darasa si kigezo cha kumfanya mwanafunzi aweze kuelewa kwa sababu alikosa sifa za kuendelea.

Kauli ya Serikali

Naibu katibu mkuu wa Tamisemi anayesimamia elimu, Gerald Mweli alisema serikali imeimarisha usimamizi wa elimu mashuleni, ikiwemo kuhakikisha wanafunzi wanafuatiliwa ipasavyo ambapo wazazi na walimu hushirikishwa.

“Hili limeenda sambamba na kuwaelimisha wazazi, walimu juu ya umuhimu wa kumsimamia mwanafunzi ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa mfumo wa kuwafuatilia wanafunzi ‘Early warning dropout system’ unaomwezesha mwalimu mkuu kugundua mienendo isiyofaa ya mwanafunzi kwa haraka,” alisema.

“Mfumo unaweza kumuambia kuwa kwa siku tatu mwanafunzi huyu hajafika shule yuko wapi, hivyo kama mwalimu anaanza kumfuatilia.”

Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Kiyange ya wilayani Buhingwe mkoani Kigoma, Samwel Moroga alisema wanafunzi wanaokaririshwa madarasa huacha shule, wengine kutokana na aibu kuwa wanakwenda kusoma na watu waliokuwa nyuma yake.

“Wakati mwingine darasa alilopo huenda mdogo wake yupo, wengine wanajisikia vibaya kuona waliokuwa nao wako mbele na wao wako nyuma, hivyo mambo mengi hutokea,” alisema Moroga.

Alisema hilo linaweza kukomeshwa pia ikiwa mzazi anaweza kumsimamia mwanawe na kuhakikisha anaendelea na shule na si vinginevyo. “Mtoto akikata tamaa ya kuendelea na shule kama mzazi anatakiwa kuendelea kumsukuma na kumpa moyo ili aweze kuendelea,” alisema Moroga.

Moroga alisema wanafunzi wengi wanaorudia madarasa ni kutokana na ufaulu wao kitaaluma kutokuwa wa kuridhisha.