Wanafunzi wenye ulemavu wakumbukwa vifaa vya shule

Muktasari:
Vifaa hivyo ni viti mwendo na baiskeli za mataili matatu tano, jozi za viatu 38 na sale za shule 40 vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la TEKLA linalohudumia watu wenye ulemavu.
Bukoba. Wanafunzi 50 wenye ulemavu kutoka Wilaya sita za Mkoa wa Kagera wamepewa msaada wa vifaa mbalimbali vya shule, viti mwendo na baiskeli vyenye thamani ya Sh17 milioni.
Vifaa hivyo ambavyo ni viti mwendo na baiskeli za mataili matatu tano, jozi za viatu 38 na sale za shule 40 vimetolewa na shirika lisilo la kiserikali la TEKLA linalohudumia watu wenye ulemavu.
Akizungumza leo Jumatano Julai 12, 2023 kwenye hafla ya ugawaji vifaa hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amewataka wazazi kuwapeleka shule watoto wao wenye ulemavu akidai kutowapeleka nikuvunja sheria na kuwakosesha haki ya msingi ya kupata elimu.
“Kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakikiuka sheria ya kuwapeleka watoto wao kuanza shule ya msingi, kwa mzazi yeyote ambaye atabainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua za kisheria, Serikali yetu imeweka mipango mizuri kwa ajili ya watoto wetu ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa vya kutosha,” amesema Sima
Mtendaji Mkuu wa shirika la TEKLA, Mugisha Kasaju amesema wanafunzi waliopokea msaada huo ni kutoka katika shule za msingi Mgeza viziwi, Mgeza Mseto, Tumaini, Rubale, Ryamaholo na Buzi.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mgeza Viziwi, Benson Rwechungura amesema wazazi na walezi wa watoto wenye ulemavu wana mwamko mdogo wa kuwapeleka watoto shule jambo ambalo linasababisha watoto hao kukosa haki ya kupata elimu.
“Tunakumbana na changamoto ya wazazi kuwa na mwamko mdogo wa kuwapeleka shule watoto wenye ulemavu,
“Mfano watoto wanapofunga shule baadhi ya wazazi hawaji kwa wakati kuwatafuta watoto wao shule kuwapeleka nyumbani na wanapofungua shule baadhi ya wazazi wanachelewa kuwarudisha shule kwa madai kwamba wanaanza kuwahudumia vifaa vya shule wale watoto wao ambao si wenye ulemavu,” amesema
Mmoja wa mzazi mwenye mtoto mwenye ulemavu, Autropia Benedicto amesema mtoto wake Merry Daudi (11) yupo darasa la awali shule ya msingi Mgeza Mseto ambaye ana ulemavu wa miguu kushikana na mikono miwili kupinda.
Amesema alikuwa anabebwa kutoka bwenini kwenda darasani lakini msaada huo wa kiti mwendo utamsaidia kupunguza adha ya kubebwa kila wakati.