Wanajeshi 1,500 wa EAC kushirikia mazoezi Tanga
Muktasari:
- Askari wa majeshi ya ulinzi na usalama kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameanza mazoezi ya kijeshi jijini Tanga
Tanga. Askari 1,500 wa majeshi ya ulinzi kutoka nchini za Afrika Mashariki kesho Jumanne Novemba 6 hadi 13, 2018 wanatarajiwa kushiriki mazoezi ya pamoja jijini Tanga ambayo yamepewa jina la "zoezi la ushirikiano imara 2018."
Mkuu wa mafunzo oparesheni wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Meja Jenerali Alfred Kapinga akizungumza leo Jumatatu Novemba 5,2018 amesema mazoezi hayo yanafanyika kwa awamu mbili tofauti ambapo ya kwanza yameanza leo yatakuwa ya ndani wakati ya awamu ya pili yataanza Novemba 9 hadi 21,2018.
Amesema dhima ya zoezi hilo kwa mujibu wa mkuu huyo wa mafunzo ni kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika Mashariki katika masuala ya ulinzi na usalama kwa ujumla.
Mbali ya shughuli za ulinzi amesema askari hao pia watafanya ukarabati katika shule ya Sekondari, chuo cha Kilimo Mlingano pamoja na huduma ya tiba bila malipo kwa wananchi wote.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela amewataka wananchi watakapoona shughuli hizo za kijeshi zinaendelea wasishtuke kwani ni katika kuimarisha ulinzi na usalama wao.