Wanakijiji Iringa watakiwa kukoka moto, kutotembea usiku kujilinda na simba

Wakazi wa Kijiji cha Lupembe Lwa Senga kata ya Lwamgungwe wakizungumza na Mwananchi baada ya kijiji hicho kuvamiwa na simba aliyekula ng'ombe wawili

Muktasari:

Kutokana na hofu ya kuvamiwa na simba, Serikali ya Kijiji cha Lupembe Lwa Senga, Kata ya Lyamgungwe, wilayani Iringa imetoa rai kwa wananchi kurudi majumbani kwao ifikapo saa 11 jioni wakati jitihada za kumtafuta mnyama huyo zikiendelea.

  


Iringa. Kutokana na hofu ya kuvamiwa na simba, Serikali ya Kijiji cha Lupembe Lwa Senga, Kata ya Lyamgungwe, wilayani Iringa imetoa rai kwa wananchi kurudi majumbani kwao ifikapo saa 11 jioni wakati jitihada za kumtafuta mnyama huyo zikiendelea.

Tangu Juni 13, mwaka huu simba hao waliingia kwenye makazi ya watu katika Kata ya Maboga na Kiponzelo, vilivyo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Akizungumza na Mwananchi Digital, Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Ezekiel Mhhehe ameomba jitihada za kumsaka simba huyo ziongezeke ili kuondoa hofu kwa wananchi hao.

 “Kijijini kwetu wamekula ng’ombe wawili, tunaomba jitihada ziongezeke kwa kweli tunaogopa sana, tunachofanya nikuwasisitiza wananchi watulie majumbani hasa kuanzia saa 11 jioni. Na kweli ikifika muda huo humkuti mtu mtaani,” amesema Mhhehe.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy amesema mpaka sasa simba wanakadiriwa kuua ng’ombe 25, kujeruhi wawili, mbuzi watano, kondoo watano, nguruwe watatu na kuku mmoja.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hao wakizungumza na Mwananchi Digital jana Jumapili Juni 25, 2023, wamesema simba hao wakipatikana maisha yao yatarudi kwenye hali ya kawaida tofauti na sasa wakati hofu imetawala.

Mmoja wa wafugaji ambaye ng’ombe wake ameliwa na simba, Vitalis Kihanga amesema familia yake inahofu baada ya tukio hilo kutokea.

“Tunaomba msaada, Serikali iendelee kutafuta simba,” amesema Kihanga.

Kamishna wa Uhifadhi ya Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), William Mwakilema ni miongoni mwa viongozi walioingia vichakani kusaka simba hao.

 “Nilipata taarifa ya uvamizi wa wanyama hawa katika vijiji vilivyoko mbali kabisa na hifadhi zaidi ya kilometa 25 lakini hadi sasa simba hao wameshakwenda umbali wa zaidi ya kilometa 70,” amesema.

Amesema tayari wameshavuka barabara ya lami ya kutoka Morogoro, Iringa kwenda Mbeya na wako upande wa pili wa barabara wakiendelea kufanya uharibifu.

"Timu ya askari 17 kutoka Hifadhi ya Taifa Ruaha na maofisa kutoka Kanda ya Kusini walifika kwa haraka kushirikiana na wenzetu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Tawa na KDU kuwasaka simba hao wasilete madhara zaidi." amesema

Kessy amewasisitiza wananchi kuendelea kufuata kanuni zitakazowasaidia kujikinga na simba ikiwamo kukoka moto kwenye mazizi nyakati za usiku, kutotembea usiku na kutembea kwa makundi wakati wa kwenda na kurudi shambani.

Pia amewataka wasile mizoga mara baada ya simba kuua ng’ombe na kuondoka.

Lupembe lwa Senga ni kijiji kilicho umbali wa takribani kilometa 30 toka njiapanda ya Ihemi, barabara Kuu ya Iringa - Mbeya.