Wanakijiji Moshi walalamikia uhaba wa maji

Muktasari:

  • Wananchi wa kijiji cha Singa Kata ya Kibosho Mashariki wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wanalazimika kunywa maji yasiyo safi na salama yanayotoka katika mto Karanga, hali ambayo inahatarisha usalama wa afya zao.

Moshi. Wananchi wa kijiji cha Singa Kata ya Kibosho Mashariki wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wanalazimika kunywa maji yasiyo safi na salama yanayotoka katika mto Karanga, hali inayohatarisha usalama wa afya zao.

Wananchi hao wamesema wanalazimika kunywa maji hayo kutokana na mgao mkubwa wa huduma hiyo uliopo katika kijiji hicho,  ambapo  kwa mwezi yanatoka mara moja au wanakosa kabisa.

Wakizungumza na Mwananchi leo Februari 21,2024  wananchi hao wamesema licha ya baadhi yao kuunganishiwa maji kwa gharama ya Sh162, 000 mwaka 2018, changamoto ya kupata huduma hiyo  imeendelea kuwepo katika kitongoji na kusababisha kero.

Yasinta Mushi, mkazi wa kitongoji cha Singa kati, amesema, "haya maji sisi wenyewe ndio tumechimba miaka hiyo na baadaye tuliambiwa ukitaka kufungiwa unalipa Sh162,000 tulifanya hivyo, lakini mpaka leo hatuji hizo fedha zilienda wapi na maji hayatoki.

“Tunaomba Serikali ituangalie maana maji tumechimba wenyewe na tumechangia fedha, hatujui ziko wapi na sisi tunaendelea kuteseka," amesema.

Kwa upande wake Anna Mariki, mmoja wa wananchi wa kijiji hicho, amesema wakati mwingine wanalazimika kutembea umbali mrefu kwenda kusaka maji ya mto karanga, kwa ajili ya matumizi yao ya nyumbani ikiwemo kupikia na kunywa kutokana na changamoto ya mgao wa maji.

"Maji ni changamoto sana hapa kwetu, zinapita siku 10  na zaidi huoni maji kwenye bomba, wakati tulipofungiwa tulihakikishiwa yatapatikana muda wote  cha kushangaza imekuwa ni kinyume chake," amesema.

Mwenyekiti wa kijiji hicho, Aloyce Chuwa amesema awali wananchi wa kijiji hicho walikuwa na mradi wao wenyewe wa maji na baadaye yalitawanywa maeneo ya vijiji vingine, hali ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa wananchi hao kukosa maji.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Singa Kifueni, Joseph Ngowi amesema baada ya mradi wa maji kusimamiwa na taasisi ya Sikika ufanisi wake umekuwa mdogo.

 "Tuliletewa watu wanaoitwa Sikika kuchukua nafasi ya jumuiya watumia maji iliyokuwa hapa kijijini, mpaka sasa wananchi bado hawajaelewa hii taasisi inafanya kazi gani hapa, tumefanya vikao bila mafanikio, changamoto imeendelea kuwepo ya maji, wananchi wanaendelea kutaabika," amesema.

Akizungumzia malalamiko hayo, Meneja anayesimamia mradi wa maji kijijini hapo, kutoka taasisi ya Sikika, Mwita Juma amekiri uwepo wa changamoto hiyo ya maji katika baadhi ya maeneo kijijini hapo.

"Mafundi ambao wanahudumia mradi huu wapo watatu kuna eneo letu moja lipo Uchao kusini na Maua ndio kuna changamoto ya maji, sasa hivi tunaongeza nguvu katika maeneo hayo na baada ya kumaliza watahamia Singa ambalo lina changamoto ya maji pia, hivyo uvumilivu unahitajika," amesema.