Mradi mpya wa maji Mwanza wafikia asilimia 99

Muktasari:

  • Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa chanzo kipya eneo la Butimba jijini Mwanza wenye thamani ya zaidi ya Sh70 bilioni, kunaongeza matumaini ya wakazi wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake ya  kuondokana na adha ya maji.

Mwanza. Utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa chanzo kipya eneo la Butimba jijini Mwanza umekamilika kwa asilimia 99, huku ukionyesha mwanga wa kuondokana na tatizo la maji katika jiji hilo.

Kukamilika kwa mradi huo unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh70 bilioni kunaongeza matumaini ya wakazi wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake wanaohudumiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa) kuondokana na adha ya tatizo la maji.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wakati wa ziara ya Kamati ya Bunge ya Bajeti Januari 8,2024, Meneja wa mradi, Celestine Mahabi amesema mtambo mmoja kati ya mitano unafanyiwa majaribio.

Amesema chanzo hicho cha maji kikikamilika kitazalisha zaidi ya lita za ujazo milioni 48 kwa siku, zitakazonufaisha zaidi ya watu 450, 000 na hivyo kuongeza uwezo wa Mwauwasa katika kuzalisha na kusambaza maji.

Imeelezwa kuwa mahitaji ya maji jijini hapo ni lita milioni 172 kwa saa, hata hivyo Mwauwasa imekuwa kuzalisha lita za ujazo milioni 90 saa. Hivyo kuongezeka kwa chanzo hicho, kuitafanya mamlaka hiyo kuzalisha lita 138 kwa saa.

Mradi huo ulioanza kutekelezwa Februari, 2021 na ulipaswa kukamilika Oktoba, 2023, lengo likiwa ni kuwezesha Mwauwasa kuwa na chanzo kingine cha maji badala ya kutegemea chanzo kimoja cha Capri-Point.

Kutokana na kukamilika kwa mradi huo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameuagiza uongozi wa Mwauwasa kuharakisha kazi ya kuwaunganishia huduma wananchi huku akiweka wazi kuwa ni nia ya Serikali kuona wote wanaoishi jirani na maeneo yenye vyanzo vya maji wanaondokana na tatizo la maji.

“Moja ya changamoto ni upatikanaji wa fedha….mahitaji (ya maji kwa wakazi wa jijini Mwanza) ni lita za ujazo milioni 172 lakini uzalishaji kwa sasa ni lita za ujazo milioni 90,’’ amesema Waziri Aweso

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Amos Makalla amesema kutekelezwa kwa mradi huo kunaongeza uhakika wa kupatikana kwa huduma hiyo kwa wakazi wa Jiji la Mwanza na vitongoji vyake huku akiutaka uongozi wa Mwauwasa kuboresha miundombinu kuhakikishia siyo tu wananchi uhakika wa huduma, bali pia kupunguza upotevu wa maji.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Daniel Sillo amesema kamati hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa mrad huku akiwataka watendaji wenye dhamana ya usimamizi kutimiza wajibu wao.