Wananchi Handeni waiangukia Serikali ukarabati wa barabara

Muktasari:

Wananchi wa kata ya Kwasunga Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameiomba Serikali kukarabati barabara inayounganisha Handeni na Bagamoyo kutokana na kuwa mbovu kwa muda mrefu.

Handeni. Wananchi wa kata ya Kwasunga Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameiomba Serikali kukarabati barabara inayounganisha Handeni na Bagamoyo kutokana na kuwa mbovu kwa muda mrefu.

Wakizungumza kwenye ziara ya mbunge, John Sallu  ya kukagua miradi ya maendeleo na kutoa shukrani kwa wananchi, wamesema kata ya Kwasunga barabara zake ni mbovu na kwamba kwa miaka 15 hakuna daraja la uhakika kwenda wilaya ya jirani Bagamoyo kupata huduma.

Mmoja wa wakazi wa kata hiyo, Hussein Thabiti amesema kero ya barabara na daraja wamedumu nayo kwa muda mrefu bila ufumbuzi.

Mwenyekiti wa kijiji cha Kwasunga, Jumanne Seleman amesema, "watu watatu wameshafariki kwa ubovu wa barabara hii, walikuwa wanapelekwa hospitali ila kutokana na changamoto hii wagonjwa walikufa njiani maana Miono(Bagamoyo) ni mbali na Mkata ni mbali.”

Sallu amesema tayari ameongea na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuona umuhimu wa kuichukua na kuhudumia barabara hiyo kwa kuwa bajeti ya Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) haikidhi kuweza kukarabati barabara kutokana na bajeti yao kuwa ndogo.