Wananchi Katubuka hatarini kupata magonjwa ya mlipuko

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wakazi wa kata ya Katubuka, Manispaa ya Kigoma Ujiji wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu na Malaria kutonana na maji yaliyotuama katika bwawa la Katubuka na kusambaa kwenye makazi ya watu na barabara ya kuelekea uwanja wa ndege, hali iliyosababisha magari kushindwa kupita.

Kigoma. Wakazi wa kata ya Katubuka, manispaa ya Kigoma Ujiji wapo hatarini kukumbwa na magonjwa ya milipuko ikiwemo kipindupindu kufuatia kutuama kwa maji ya mvua kwenye makazi ya watu na barabarani yanayotoa harufu mbaya.

Eneo hilo ni maarufu kwa jina la Manguruweni kwa sababu ya kuwepo kwa machinjio na mabucha ya kuuza nyama ya nguruwe, limezingirwa na maji na kufanya wafanyabiashara kuhamia upande wa pili kukwepa.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi na wafanyabiashara wa nyama ya nguruwe  wamesema pamoja na kuhamia upande wa pili kuyakwepa maji, lakini yanatoa harufu na kuhofia usalama wa  biashara yao hasa suala la afya.

Mfanyabiashara, Jackson Mathayo amesema wanaiomba Serikali kuwaondolea maji hayo au kuwatafutia eneo lingine la kufanyia  biashara zao, kwani sehemu hiyo si salama tena kwa walaji wao na kwa sasa hawapati wateja kama ilivyokuwa awali.

Mkazi wa Katubuka, Joram Yohana amesema mbali na maji hayo kutoa harufu mbaya pia kumekuwa na mbu wengi sana kwa wakazi wa maeneo ya karibu, hivyo ni vema Serikali ikaona namna ya kufanya kuyaondoa.

“Maji yanatoa harufu hasa kwa sisi wa karibu na eneo hili kutokana na kuchanganyika na maji ya vyooni na bwawa la katubuka lakini mbu wameongezeka, hii ni hatari sana na hofu yetu kubwa ni magonjwa ya milipuko na Malaria na ukizingatia tuna familia na watoto,”amesema Yohana.

Naye Sayuni John amesema changamoto ya maji kujaa eneo hilo na kuhamia eneo lingine upande wa pili imewapa hofu ya kushindwa kurejesha pesa za mikopo walizochukua benki kwa ajili ya kuendesha biashara.

Amesema anashindwa namna ya kuhudumia watoto wake ipasavyo na anaiomba Serikali iwasaidie eneo jingine la kufanyia biashara yao, kwani anaamini kuwa maji yaliyopo ni mengi na hayawezi kukauka ndani ya muda mfupi.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Jesca Leba amesema timu ya wataalamu wa afya wamefika katika maeneo hayo na kutoa maelekezo kwa wafanyabiashara hao, huku wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakiendelea kusimamia kuhakikisha kuwa kile walichoelekezwa kinafanyiwa kazi.

Diwani wa kata ya Katubuka, Moshi Mayengo amesema kwa sasa wananchi wameomba hifadhi kwa ndugu na majirani kwa muda, wakati wakiendelea kusubiri hatua zitakazochuliwa na Serikali.

Amesema tangu mkuu wa wilaya alipoenda wakati wa tukio la nyumba kuingiliwa na maji Serikali ipo kimya, ingawa kwa upande wa eneo la barabara iliyojaa maji tayari Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), wameanza taratibu za kutoa tope kwenye bwawa hilo.