Wananchi Kawe wahoji utekelezaji ahadi za Askofu Gwajima

Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima.

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wa Kawe wamehoji kuhusu utekelezaji wa ahadi alizotoa mbunge wao, Askofu Josephat Gwajima wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2020.

Ahadi ni deni, ndivyo wasemavyo Waswahili. Ukiwa ni mwaka wa nne akiwa madarakani, baadhi ya ahadi hazijatekelezwa.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi mapema wiki iliyopita, Askofu Gwajima ambaye pia ni kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, amesema zipo zilizotekelezwa na kwamba kwa kuwa muda bado upo wasubiri waone utekelezaji.

Amesema yeye ni mtu maarufu, ndiyo maana ahadi zake zinauliziwa sana.

“Katika hili mtu anayetulaumu ni mjinga tu, sababu huwezi kumlaumu mtu na muda wake wa uongozi bado haujaisha kwani bado tuna mwaka mzima. Kwa hiyo, mtu anayelaumu ni mjinga tu au ni siasa tu,” amesema.

Hivi karibuni picha jongefu (video) za ahadi zake zilivuma mitandaoni zikimwonyesha akihutubia katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

“Mimi nikichaguliwa kuwa mbunge, nitaleta boti za uvuvi kwenye jimbo la Kawe, halafu vijana wetu wote tutawafungulia chuo cha uvuvi, kwa sababu jimbo la Kawe lina neema lipo karibu na bahari ambayo haijatumiwa na wenyeji.”

“Kwa hiyo jambo la kwanza vijana wetu watakwenda kujifunza kuendesha boti, jambo la pili watajifunza kukarabati, kwa mfano boti imeharibika na jambo la tatu watajifunza kuvua kwa kutumia boti,” hizo ni baadhi ya ahadi za Askofu Gwajima.

Pia aliahidi kupeleka vijana wa jimbo hilo katika Jiji la Birmingham nchini Uingereza, akisema kutakuwa na programu za mafunzo za kubadilishana wanafunzi.

Bunge lampa adhabu Askofu Gwajima

Wavuvi wafunguka

Akizungumza na Mwananchi Januari 26, mwaka huu, Ernest Gabriel, mvuvi katika eneo la Kunduchi, amesema tangu mbunge huyo alipoahidi, hawajamuona na wanaendelea kupambana kuvua kwa zana duni.

“Nitumie fursa hii kuwashauri wabunge wote, kila wanapowaahidi wananchi wawe wanatekeleza, kwa kuwa unapomdanganya mtu mzima kuwa utamletea pipi, lazima akuhoji utakapokuja mara nyingine kuomba kura, nini ulitekeleza katika ahadi zako?” amehoji.

Amesema kwa vyombo duni walivyonavyo, hawawezi kujiita wavuvi bali wadundulizaji, huku akitaka mamlaka na viongozi kuwaiga Zanzibar ambao kutokana na kampeni yao ya uchumi wa buluu, hivi sasa wavuvi wa huko wana zana za kisasa, zikiwamo boti.

Kwa upande wake, Said Hassan, mwenye uzoefu wa miaka 30 katika kazi ya uvuvi, amesema hakuna mpango uliofanyika kuwawezesha kupata boti mpya kama alivyowaahidi mbunge wao.

Hassan amesema katika kipindi hiki ambacho samaki wanapatikana mbali, wana uhitaji mkubwa wa kuwa na boti za kisasa, hata za kukopeshwa kwa kujiunga vikundi vya watu watatu hadi watano.

Naye Ditrick Haule, amesema kuna siku walifika kwao watu waliojitambulisha wanatoka serikalini waliowataka wajiandikishe kwenye vikundi ili wakopeshwe boti, lakini mpaka leo imekuwa kimya.

“Ukiwa na boti ya kisasa hata nusu saa haumaliza unakuwa umeshawafikia samaki,” amesema mvuvi huyo.

Akizungumzia ahadi hiyo, Askofu Gwajima amesema: “Suala la boti kata zangu zote nne, kwa maana ya kata za Msasani, Kawe, Kunduchi na Mbweni zipo baharini na zote hizo zina wavuvi.”

Amesema zana za uvuvi jimboni humo ni jambo halisi kwa sababu linahusu wana-Kawe wa kata zote nne na sehemu moja ya Bunju.

“Mtu asubiri mpaka mwisho kuona kazi yetu ya ubunge, ataona matokeo, hayo ni maneno nayoweza kusema kwa sasa,” amesema.

Askofu Gwajima ataka tafsiri ya maendeleo

Ujenzi wa shule Chasimba

Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa, Askofu Gwajima anasema ni ujenzi wa Shule ya Msingi Chasimba, uliogharimu zaidi ya Sh70 milioni.

Mwananchi limefika eneo hilo na kushuhudia shule yenye jengo moja lenye madarasa mawili na ofisi moja.

Pia kuna jengo la vyoo ambavyo havijakamilika, hivyo shule hiyo bado haijaanza kutumika.

Mjumbe wa Mtaa wa Basihaya, Khadija Mustafa amesema shule hiyo ilijengwa baada ya wananchi kulalamika kuwa wanafunzi wanatembea umbali mrefu kufuata shule Kata ya Boko.

“Mbunge alipokuja kututembelea tulimweleza kero yetu ya wanafunzi kutembea umbali mrefu. Utakuta mtoto wa darasa la kwanza anatembea kutoa Basihaya hadi Boko, anachoka, ndipo akatujengea pale,” amesema.

Hata hivyo, amesema Serikali ina mpango wa kujenga shule kamili katika eneo hilo.

Askofu Gwajima amesema mradi mwingine uliotekelezwa ni ujenzi wa daraja la kuvuka watu lenye thamani ya Sh94 milioni eneo la Mbopo.

Katika eneo la Mbopo kwa Mama Kapera, Mwananchi limeshuhudia daraja ambalo wananchi walichangia kalavati saba idadi sawa na yaliyotolewa na mbunge.

Akizungumzia ujenzi huo wiki iliyopita, mjumbe wa shina namba saba Kata ya Mbopo, Ermenillde Kapera amesema awali walikuwa wanataabika kutokana na maji ya mto kufurika nyakati za mvua.

Askofu Gwajima ahojiwa akiwa amesimama

“Niliitisha kikao baada ya kuona njia yetu wakati wa masika hatuvuki, wala watoto hawaendi shule, wala wanawake hawaendi kujifungua. Hivyo tukaamua kuchangishana, wengine Sh10,000 wengine Sh20,000, hadi tukanunua kalavati saba, amesema na kuongeza:

“Tulipoona uwezo wetu umefika mwisho, nikafikiri tutajengaje? Tukasikia wiki ya pili, mbunge wetu anafika eneo letu kujenga daraja na mimi nikajitosa kwenye mkutano wake.”

Amesema baada ya Askofu Gwajima kuhutubia alikaribisha wenye kero, ndipo yeye akaeleza kuhusu ujenzi wa kalavati.

“Nikawa wa kwanza kunyoosha mkono, akanipokea, nikasema shida yangu kubwa njia yetu haipitiki wakati wa masika, tunaomba msaada. Akaniambia mama kesho uje hapa saa moja asubuhi,” amesema.

Amesema kesho yake alipofika muda huo alikuta wasaidizi wa mbunge na mtaalamu kutoka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) waliopima eneo hilo na kuondoka.

“Ndani ya mwezi mmoja, mbunge akaibuka. Nikapigiwa simu, mama kafuate greda Tegeta, nikaenda greda likaja likachonga barabara,” amesema.

Amesema pia mbunge aliwaletea kalavati saba, hivyo zikafika 14 na zikajengwa.

Hata hivyo, kutokana na mvua za el-nino kunyesha hivi karibuni, amesema kalavati zimezidiwa, huku barabara pacha inayoelekea Bunju kutoka Mbopo ikiharibika kwa kukosa daraja.

“Hali yetu bado ni mbaya kwa sababu hatuna daraja katika barabara ya kwenda Bunju kutoka Mbopo na maji yamejaa kwenye makazi ya watu,” amesema Mama Kapera.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mbopo, Ally Mziwanda amesema mbunge wao licha ya kuwezesha ujenzi wa kalavati la Mama Kapera, pia amefanikisha wa daraja la Pangaboy lililokuwa limesombwa na mafuriko.

“Alichofanya ni ufuatiliaji, aliwapigia simu wenyeviti wa serikali za mitaa na kuwauliza changamoto zao, tunashukuru Mkuu wa Mkoa alifika, Mkuu wa Wilaya, Tarura walifika na walijenga,” amesema.

Amesema pia wameahidiwa kutajengwa daraja katika barabara ya Mbopo -Bunju ifikapo Aprili.

Mziwanda amesema mbunge amewezesha ujenzi wa hosteli ya Shule ya Sekondari Mbopo na upatikanaji wa mradi wa maji.

Askofu Gwajima ahoji masheikh kushikiliwa bila kesi kufikishwa

Ujenzi wa mtaro

Askofu Gwajima amesema amejenga mtaro wa mita 300 katika Kata ya Msasani uliogharimu Sh171 milioni kwa lengo la kuondoa maji kwenye makazi ya watu.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Msasani, Elizabeth Minga amekiri kujengwa mtaro huo, akisema umesaidia kupunguza mafuriko.


Kuhusu kupeleka vijana Birmingham nchini Uingereza, Askofu Gwajima amesema ahadi hiyo inapotoshwa na baadhi ya watu kwani ahadi yake haiwahusu wakazi wote wa jimbo hilo.

“Kwa kutojua tu watu katika hili wanasema niliahidi kwamba wananchi wote wa Kawe nitawapeleka Birmingham, ndugu mwandishi naomba urejee vizuri hiyo clip kile nilichosema,” amesema.

Amesema jimbo la Kawe lina uhusiano mzuri na Halmashauri ya Birmingham.

“Nikasema kawaida wanafunzi wanaweza kufanya exchanging programs na hiyo ni furaha yangu, hivyo endapo itatokea programu hiyo nitasimamia na wanafunzi watafanya,” amesema.

Mbwembwe za Askofu Gwajima akiomba kura

Miongoni mwa ahadi za mbunge huyo ni kununua greda kwa ajili ya ujenzi wa barabara za jimbo hilo.

“Ulikuwa unasikia ooh greda, greda ipo. Mimi nakaa hapa Salasala ukiwa na muda twende, tumenunua greda lipo tunasubiri liingie kazini,” amesema.

Wakati Gwajima akisema hayo, Januari 19, 2024 Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Paul Makonda aliahidi kukabidhi katapila 20 kwa mbunge huyo kusaidia ujenzi wa barabara za mitaani.

Alitoa ahadi hiyo kutokana na malalamiko ya wananchi wa kuhusu ubovu wa barabara.

Akizungumzia hilo, Gwajima amesema wameamua zisubiri kwanza mvua zipungue.

“Kwa hiyo nawasihi wananchi wawe watulivu, si rahisi ukapitisha greda mahali penye tope itakuwa matatizo zaidi. Tutulie kidogo, likitokea jua na kuondoka hali ya uteke (tope), tutawasaidia wananchi,” amesema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Hanifa Hamza, amesema ipo miradi aliyotekeleza Askofu Gwajima kwa fedha zake za mfukoni na kwa fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Jimbo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.

"Kama ambavyo umekwenda kwa watendaji wa mitaa na wamekuonyesha baadhi ya miradi aliyotekeleza mbunge huyo, wale ni wakurugenzi katika mitaa yao, hivyo wanachosema ndivyo kilivyo," amesema.