Askofu Gwajima: Spika Ndugai jiuzulu

Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima

Muktasari:

Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima amemshauri Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kwamba hataweza kuliongoza Bunge kwa sababu wabunge wote watakuwa upande wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Dar es Salaam. Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima amemshauri Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiuzulu nafasi hiyo kwa madai kwamba hataweza kuliongoza Bunge kwa sababu wabunge wote watakuwa upande wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Askofu Gwajima ameyasema hayo leo Alhamisi Januari 6, 2022 jijini Dar es Salaam wakati akitoa maoni yake kuhusu kauli ya Spika Ndugai kuhusu mikopo aliyoitoa Desemba 28, 2021 wakati akizungumza kwenye mkutano jijini Dodoma.

Katika mkutano huo, Spika Ndugai alisema kukopa kunaongeza mzigo kwa wananchi na kwamba sasa ni wakati wa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia tozo mbalimbali zilizoanzishwa bila kutegemea mikopo.

Alisisitiza kwamba deni la Taifa limepaa hadi kufikia Sh70 trilioni, hali ambayo inatisha na kwamba siku moja nchi "itakuja kupigwa mnada" kwa sababu ya madeni.

Akizungumzia kauli hizo za Spika Ndugai, Askofu Gwajima amesema kauli hiyo ina nia ovu kwa sababu alikuwa na nafasi kubwa ya kushauri na kutoa maoni yake ya namna bora ya kuendesha nchi bila mikopo.

Amesema suala ya mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilipita bungeni katika kamati ya bajeti Oktoba 6 - 7 na likapitishwa, hivyo anashangaa Spika Ndugai kushindwa kutoa maoni yake wakati ule.

"Nashangaa kuona bosi wangu naye anazungumzia mkopo huo wakati ulipita kwenye kamati ya bunge na kamati ndiyo mikono ya Spika Ndugai," amesema Askofu Gwajima.

Amesema Spika Ndugai ni mjumbe wa kamati kuu, angeweza kuhoji suala la mkopo kwenye kikao Cha kamati kuu kilichokaa Desemba 17 ambapo angepata fursa ya kueleza hoja yake kwa wajumbe.

Vilevile, Askofu Gwajima amesema Spika Ndugai angeweza kukutana na Rais Samia na kumshauri kuhusu mikopo badala ya kwenda kuzungumza kwenye mkutano huko.

"Namshauri Spika Ndugai ajiuzulu, aachie nafasi Watanzania wengine waongoze...kwa sasa hataweza kufanya kazi na wabunge, wote tutakuwa upande wa mama," amesema Askofu Gwajima.

Amedai kuwa kauli ya Spika Ndugai ililenga kumdhoofisha Rais Samia katika utendaji wake ili akipoteza mwelekeo basi watumie fursa hiyo kwa manufaa yao ya kisiasa.